Makala

TAHARIRI: BBI: Viongozi wasitugawanye

November 8th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

KITENGO CHA UHARIRI

VITA baridi na migawanyiko ambayo imeanza kuikumba ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI) si dalili nzuri kwa umoja wa nchi.

Imebainika baadhi ya viongozi hawajaridhishwa na baadhi ya mapendekezo ya ripoti hiyo, lakini wamekuwa wakiogopa kujitokeza wazi ili kutoonekana kukiuka misimamo ya mirengo ya kisiasa wanayoegemea.

Migawanyiko hiyo ilianza mapema wiki hii, baada ya Meja Mstaafu John Seii, ambaye alikuwa miongoni mwa wanajopo 14 waliosimamia mchakato huo, kudai walishurutishwa kutia saini ripoti, licha ya uwepo wa baadhi ya mapendekezo ambayo hayakuwaridhisha.

Kauli yake ilizua hisia mseto, huku baadhi ya wanachama wakikanusha vikali madai hayo kuwa “uongo”.

Baadaye, mwanajopo huyo alibatilisha kauli yake, akisema “alinukuliwa visivyo” na vyombo vya habari.

Bila shaka, kinachojitokeza ni kuwa kuna sehemu kubwa ya watu walioshiriki kwenye mchakato wa maandalizi ya ripoti, ambao hawakuridhishwa na ujumuishaji wa mapendekezo yaliyopo, lakini wanaogopa kujitokeza kueleza wazi.

Ikizingatiwa hii ni ripoti muhimu, inayolenga kuleta mageuzi kwenye mpangilio wa kisiasa nchini kati ya masuala mengine mazito, ni kosa kuu ikiwa kuna baadhi ya washiriki walizuiwa kutoa kauli zao.

Tangu mwanzo wa mchakato wa maandalizi ya ripoti hiyo, Wakenya waliamini uliendeshwa kwa maelewano makubwa kati ya wanajopo wote.

Hili ni kulingana na taswira, semi na matamshi ambayo yalikuwa yakitolewa na washiriki kila mara walipopata nafasi kuwaeleza Wakenya kuhusu hatua walizopiga.

Ikizingatiwa jopo hilo liliwashirikisha watu wa hadhi kama Seneta Yusuf Haji wa Garissa, kila Mkenya alitarajia wanajopo wangetumia tajriba zao kusuluhisha tofauti zilizoibuka.

Wito wetu sasa ni kwa Rais Uhuru Kenyatta na kinara wa ODM, Bw Raila Odinga, kuhakikisha mchakato huo haugeuki kuwa jukwaa la malumbano mapya, kwani hilo litakuwa sawa na kuturejesha nyuma.

Kabla ya kuwasilishwa kwa wananchi kupigiwa kura ya maamuzi, tunawaomba wawili hao watoe mwanya kwa watu wanaohisi kauli zao hazikuzingatiwa kutoa hisia zao bila pingamizi zozote.

Hilo ndilo litahakikisha mchakato huo umetimiza lengo lake kuu, kuwaunganisha Wakenya bila kuwatenga wengine.