TAHARIRI: CAK yapaswa ikabili matusi mitandaoni
KITENGO CHA UHARIRI
MWAKA wa 1999 ulimwengu ulipojiandaa kukaribisha Milenia, kulikuwa na wasiwasi kote ulimwenguni.
Hofu hii ilitokana na uvumi kuwa Milenia ingekaribisha ulimwengu wa utandawazi ambapo kompyuta zingetawala na kuwanyima ajira mamilioni ya watu kote ulimwenguni.
Badala yake, ulimwengu ulishuhudia kuundwa kwa apu kama vile Yahoo, Hotmail, Skype na kadhalika, zilizorahisisha mawasiliano.
Simu za mkononi pia zilianza kuuzwa na kampuni kama Erickson, Nokia, Motorola, Sagem na kadhalika.
Katika mwongo mmoja uliopita, kumeundwa simu za kisasa pamoja na mitandao kama Facebook, Twitter na WhatsApp. Ingawa mitandao hii imesaidia kupanuka kwa sekta ya mawasiliano, kwa bahati mbaya watu wengi hapa Kenya wamekuwa na wanaendelea kuitumia vibaya.
Jambo hili si tatizo la Kenya pekee. Rais Donald Trump wa Marekani amekuwa miongoni mwa watu walio mstari wa mbele ulimwenguni, kujieleza na kueneza hisia zake kupitia mtandao wa Twitter. Bila kujali kama maneno yake yatachoma nafsi za wengine au la, Rais huyo husema anachotaka na kuwakabili maadui wake bila kupumzika.
Mkenya aliye uhamishoni nchini Canada, Miguna Miguna ni mwingine ambaye huwatusi wanaomkosoa anapomwaga hadharani aibu za watu wengine.
Hapa nyumbani, wakati mmoja ilimlazimu hata Rais Uhuru Kenyatta kujiondoa mitandaoni. Wakenya wenye utovu wa nidhamu walikuwa wakimkejeli na hata kumtusi kila alipoandika chochote.
Uhuni huu kupitia mitandao sasa umefikia kiwango ambapo watu hutukanana bila ya kujali nafasi walizo nazo katika jamii. Matusi haya huendelezwa kwa njia inayoibua maswali kuhusu maadili yetu kama Waafrika.
Mila na tamaduni zetu ni kwamba mzee, kiongozi na mtu mwenye mamlaka anastahili kuheshimiwa na yeye awaheshimu walio chini yake. Kutokana na uhuru mkubwa unaotolewa na mitandao, hasa Twitter, imekuwa vigumu sana mtu kutofautisha kati ya kiongozi na mlalahoi.
Kenya imeendelea kiteknolojia kutokana na utekelezaji wa teknolojia ya mawasiliano. Lakini maendeleo bila ya ustaarabu ni bure. Tume ya mawasiliano nchini (CAK) ina jukumu la kuzungumza na wasimamizi wa Twitter, waje na mfumo utakaowadhibiti wanaochapisha maneno ya matusi.