Makala

TAHARIRI: Dini zote zahimiza kuyalinda maisha

January 14th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

NA MHARIRI

KILA mwanadamu ana haki ya kuabudu anavyotaka.

Hapa Kenya, wananchi wana uhuru wa kufuata dini mbalimbali. Hata wale ambao hawaamini kuwepo kwa Mwenyezi Mungu, wana uhuru wa kufanya hivyo bila ya kuingiliwa na yeyote.

Tumeweka ndani ya Katiba, haki za watu kufanya ibada zao wakiwa huru. Imani hizi pia zinaambatana na baadhi ya tamaduni, maadamu haziingiliani na haki za watu wengine.

Wikendi tulionyeshwa kwenye runinga kisa ambapo shule moja ya upili ilimfukuza mwanafunzi aliyejiunga na kidato cha kwanza kwa msingi kuwa anafuata dhehebu la Rastafarian.

Ingawa urasta hautambuliwi kuwa dini hapa Kenya, utamaduni wa wafuasi wa Rastafarian kufuga manywele unajulikana tangu enzi za waimbaji muziki wa reggae kama marehemu Bob Marley.

Hata mahakama zetu zinafahamu kuwa shule zina uwezo wa kutekeleza na kuhakikisha sheria za taaisi zinafuatwa.

Lakini iwapo mtoto alisoma hadi darasa la nane katika shule ya msingi ya umma akiwa na nywele zake, na hazikuathiri masomo wala wanafunzi wenzake, hakuna sababu kwa shule ya upili kumlazimisha azikate au atafute shule nyingine.

Katika suala hili la Imani, serikali na viongozi wa dini wana jukumu la kuwahamisha wafuasi wa baadhi ya madhehebu kuhusu umuhimu wa kutafuta matibabu.

Katika kaunti ya Nyeri, mwanamume alifariki baada ya kukataa kuongezewa damu mwilini kwa madai kuwa imani yake ya kidini haikumruhusu kufanya hivyo.

Inasemekana kuwa madaktari walikuwa wameshauri kwamba kwa kuwa mgonjwa huyo alikuwa na kiwango cha chini cha damu, alihitaji kuongezewa kabla ya kufanyiwa uchunguzi wa figo.

Mgonjwa alikataa katakata na kusema kuwa ni haramu kwa muumini kuongezewa damu ya mtu mwengine.

Muumini huyo wa dhehebu la Jehova’s Witness alidai kuwa Bibia inaharamisha kuongezwa damu.

Yapo madhehebu mengine kama vile Kanitha wa Ngai na Kavonokya ambayo pia yana itikadi za kukataa chanjo na tiba za kisasa.

Imani za watu si jambo rahisi kuzibadili, lakini serikali yapaswa kuhamasisha watu kwamba inapofika hali ya kuwa ni kuokoa uhai, watu yafaa, ikiwezekana washasishiwe kutibiwa.