TAHARIRI: Dudu la utumiaji pufya litatuumiza
Na MHARIRI
Mashindano ya riadha za dunia yanapoingia siku yake ya pili leo Jumamosi, Kenya yafaa kulimakinikia zaidi tatizo la utumiaji wa dawa za kusisimua misuli maarufu kama pufya.
Mapema wiki hii runinga moja nchini Ujerumani ilipeperusha makala kuhusu madai ya utumizi wa pufya miongoni mwa wakimbiaji wa Kenya.
Kufuatia ripoti hiyo, Shirikisho la Riadha Duniani (IAAF) lilitangaza onyo kali kwa mataifa yanayoruhusu matumizi ya dawa hizo miongoni mwa wakimbiaji wake na hasa Kenya ambayo ni kati ya nchi maarufu zaidi katika mchezo huo duniani.
Shirikisho hilo liliahidi kulichunguza suala hilo na kusema kuwa iwapo itapatikana kuwa Shirikisho la Riadha Kenya (AK) linaendekeza uovu huo, basi hatua kali ya kinidhamu itachukuliwa dhidi yake.
Hili ni tatizo linalofaa kuchukuliwa kwa uzingativu mkuu hasa kutokana na hali ya wanariadha kadhaa wa Kenya kupigwa marufuku baada ya kugunduliwa kuwa wamekuwa wakitumia pufya wanapoelekea katika mashindano ya kimataifa.
Hivyo basi, mashirikisho ya mchezo huo nchini yanafaa yaweke mikakati thabiti ya kuzuia wanariadha wake kujiingiza katika uhalifu huu unaotishia kuchafua sifa ya Kenya.
Kadhalika, iwapo ripoti kuwa wapo viongozi wa AK au hata Kamati ya Olimpiki nchini wanaowasaidia wanariadha kupata na kuzitumia dawa hizo, wanafaa wakome upesi, vinginevyo, fahari yetu itatoweka.
Kwingineko, wanariadha wetu walioelekea Doha, Qatar kwa michezo hiyo iliyoratibiwa kuanza jana, watunzwe vizuri mbali na kujiweka katika hali nzuri itakayowawezesha kung’aa.
Ni matarajio yetu kwamba kila mmoja atapewa malipo yake kwa wakati ufaao huku makocha wakiendelea kuwapa mbinu zitakazowawezesha kushindana kwa ustadi dhidi ya miamba wa dunia.
Aghalabu wanariadha wetu hushindwa katika baadhi ya mbio kutokana na mbinu mbovu za ushindani hasa katika mbio za masafa marefu na kadri, mathalani mbio za mita 10,000 na 5,000.
Utawaona wengi wakianza mbio hizo kwa kasi zaidi wasijue kwamba mahasimu wanawasubiri wachoke halafu wawapite. Hatimaye Kenya hupoteza mataji ya masafa hayo hasa miongoni mwa wanaume. Tunatumai mara hii makocha wamewapa wakimbiaji wetu mbinu mwafaka za kupambana na hata kushinda mahasidi hao wetu.