TAHARIRI: FKF isikize wadau kuzuia malumbano
Na MHARIRI
BODI ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Nchini FKF imetangaza kuwa uchaguzi kwa nyadhifa mbali mbali kote nchini, utafanyika kati ya Septemba 19 na Oktoba 17 huku kilele kikiwa uchaguzi wa Rais.
Lakini muda mfupi tu baadaya ya tangazo hilo kutolewa na mwenyekiti Kentice Tikolo, malumbano yamezagaa kutoka kwa wawaniaji mbali mbali haswa wale wanaomezea nafasi ya Nick Mwendwa.
Malalamishi yao makuu ni kwamba la kwanza bodi hiyo haikuundwa kisheria, wakisema kwamba iliteuliwa na Mwendwa wakati ambapo muda wake wa kuhudumu ulikuwa unakwisha. Aidha, wengine wanalalamika kwamba bodi hiyo haikushauriana na wahusika wote wa mchezo wa soka kabla ya kutangaza mwongozo mpya wa uchaguzi.
Mengi ya malalamishi haya yana mashiko lakini wakosoaji pia wanafaa wakumbuke kuwa kwenye suala la muda wa kuhudumu wa Mwendwa, sheria inamkubalia kusalia mamlakani hadi pale rais mpya atakapopatikana.
Na ujio wa janga la corona uliofuta ratiba zote za michezo umemshuhudia akiendelea kuhudumu.
Ingawa mahakama ya kutatua mizozo ya kimichezo ilimtaka ashirikishe kamati huru kuteua bodi nyingine ya uchaguzi kufuatia kufutiliwa mbali kwa kura zilizofanyika Marchi, ni wazi kwamba usimamizi wa FKF uliamua kusalia na bodi waliyoteua Februari. Ingawa huu ni msingi halali wa malumbano, wawaniaji wanafaa wakumbuke kwamba ilivyo kwa sasa, ni bodi hii hii itakayofanya uchaguzi kwa sababu ki uhalisia, haijavunja sheria zozote za utendakazi wao.
Sawa na ilivyo kwenye siasa za urais wa nchi, kiongozi aliye uongozini ndiye mara nyingi anateua bodi itakayofanyisha uchaguzi utakaomdumisha au kumng’atua uongozini na ni jambo linalozua manung’uniko kwa sababu huchukuliwa kuwa wanaoteuliwa watakuwa ‘waaminifu’ kwa aliyewateua.
Kwa hivyo, wawaniaji hawa wanapolia, wana kila sababu ya kufanya hivyo. Lakini tunaishi katika ulimwengu halisi. Hawataishi kulalamika milele. Lazima maisha yaendelee. Lazima uchaguzi ufanyike.
Njia nyingine labda ni kushinikiza serikali ivunjilie mbali bodi au shirikisho hilo kwa ujumla. Lakini hatua hiyo italeta matatizo makubwa kutoka FIFA inayokataza serikali za mataifa wanachama kuingilia shughuli za shirikisho.
Njia iliyobaki ni wadau kuangalia mbinu za mjadala baina yao na shirikisho hilo ili kuona jinsi uchaguzi utafanywa kwenye mazingira ya haki na usawa. Bodi hiyo ya Tikolo nayo ifahamu ina wajibu wa kufanya uchaguzi wa wazi kwa manufaa ya soka na wananchi.