TAHARIRI: FKF yafaa iache kiburi na majitapo
KITENGO CHA UHARIRI
NICK Mwendwa aliyechaguliwa kuongoza, kwa muhula wa pili, Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) kwenye uchaguzi uliojaa utata, ameanza awamu yake hii mpya kwa maamuzi yanayoshangaza na kusikitisha wengi wanaopenda kandanda nchini Kenya.
Kinara huyo amedhihirisha kwamba hana sifa faafu za uongozi kwa matendo yake mawili ya kugutusha hata kabla ya kumaliza miezi miwili tangu achaguliwe upya katika mchakato wa kura unaoweza kunasibishwa na shindano la farasi mmoja; sharti awe mshindi.
Alianza kwa kumfuta ghafla kocha wa Harambee Stars, Francis Kimanzi pamoja na benchi lake lote la kiufundi akiwemo naibu wake Zedekiah ‘Zico’ Otieno.
Majuzi zaidi amewazuia baadhi ya wanahabari kuingia kwenye uwanja wakati wa mechi ya Ligi Kuu ya Kenya (KPL) kwa sababu zisizojulikana, ila kilichojitokeza wazi ni kuwa anajaribu kulazimisha vyombo hivyo vya habari kuepuka kuangazia udhaifu wake na shirikisho hilo analoongoza.
Hatua hiyo ilimsawiri Mwendwa kama mwenye kiburi na majitapo anayetawaliwa na fikra kwamba maadamu yuko kwenye usukani hakuna linaloweza kumtisha hata afanyapo maovu.
Baada ya kumfuta kocha Kimanzi, alimkabidhi mikoba kocha wa zamani ambaye kwa sasa ni mtangazaji katika mojawapo ya idhaa za redio nchini; mkufunzi Jacob ‘Ghost’ Mulee.
Hatusemi kwamba Mulee hawezi kazi maadamu amewahi kuongoza na kuwezesha timu hiyo kupiga hatua ya kujivunia katika mashindano ya kimataifa, bali makali ya kocha huyo yanatiliwa shaka kutokana na hali kwamba umakinifu wake wote haupo kwenye soka pekee bali katika shughuli nyinginezo.
Aidha, hali aliyomfuta kocha Kimanzi ilijitokeza kama siasa chafu ambazo zinaendelea katika shirikisho hilo, na ambazo zisipodhibitiwa huenda zikadidimiza kabisa ndoto ya Kenya kufufua fani ya kabumbu.
Sharti Mwendwa aanze kujisaili na kutafakari kwa kina mkondo anaotoka kuelekeza kandanda yetu.
Kenya imekuwa na maono ya kufuzu kwa Kombe la Dunia angaa kwa mara ya kwanza pamoja na kuendelea kuingia katika fainali za Kombe la Afrika mara nyingi iwezekanavyo.
Matamanio haya hayawezi kufikiwa iwapo siasa chafu, kiburi na majigambo ndiyo yatakayokuwa falsafa ya viongozi wa FKF.