TAHARIRI: Fujo uwanjani zinavuruga soka
Na MHARIRI
JOPO Huru la Nidhamu na Malalamishi la KPL linapaswa kuungana bega kwa bega na maafisa wa kulingana usalama kupiga vita fujo zinazotokea mara kwa mara viwanjani.
Ni majuzi tu ambapo mashabiki walihatarisha misha yao kule Awendo baada ya mechi kati ya wenyeji, SoNy Awendo na AFC Leopards, lakini kufikia leo, jopo hilo halijatoa uamuzi wotote.
Msimu huu, zaidi ya mecho tano za Ligi Kuu ya Kenya zimevurugwa na mashabiki wapendao fujo, lakini hawaadhibiwi ipasavyo.
Mechi ya Awendo ilitibuka dakika ya 68 kufuatia mvua nyingi iliyonyesha katike sehemu hiyo wakati Leopards wakiongoza kwa 1-0.
Kulingana na sheria, mechi hiyo ilitakiwa kurudiwa siku iliyofuata, asubuhi, lakini kutokana na fujo za mashabiki wa timu ya nyumbani haikuchezwa.
Leopards waliwasili uwanjani lakini wakakataa kucheza baada ya Sony kupuuza sheria za KPL.
Kati ya mambo muhimu yaliyofanya wakatae kucheza ni kutohakikishiwa usalama, kwani ni maafisa wanne pekee waliokuwa uwanjani humo mechi ilipotarajiwa kuanza.
Kisheria, mechi yoyote inayohusu timu ya mashabiki wengi kama AFC Leopards na Gor Mahia, lazima kuwe na angalau maafisa wa polisi 20.
Kadhalika, lazima kuwe na ambulensi na vifaa hitajika, mbali na madaktari wa kutosha kuwahudumia wachezaji au mashabiki wanaoumia.
Ingawa wakuu wa klabu ya SoNy walikanusha madai kwamba ndio waliosababisha kutochezwa kwa mechi hiyo, uwanja wa Awendo haufai kuchezewa mechi yoyote ya ligi kuu kutokana na udogo wake, mbali na uharibifu wa kila mara wakati wa mvua kubwa.
Mbona wasipeleke mechi zao Moi Stadium Kisumu katika uwanja ambao una kila kitu kinachohitajika, mbali na mkeka ambao hata mvua ikinyesha kiasi gani, mechi itachezeka?
Kulingana na maafisa wa Ingwe waliokuwa Awendo kwa ajili ya mechi hiyo, ambulensi ya SoNy ilikosa kifaa fulani muhimu ambapo Ingwe walisisitiza lazima kiwepo.
Kadhalika Leopards walitaka idadi ya maafisa wa polisi iongezeke ili mechi ichezwe katika mazingara yanayofaa.
Tunatarajia KPL kuwapa Ingwe ushindi wa mabao mawili na ponti tatu, mbali na kuiadhibu timu ya Sony ambayo mashabiki wake wamezoea kuvuruga mechi.