• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 3:55 PM
TAHARIRI: Heko Serikali kuokoa timu za Gor, Starlets

TAHARIRI: Heko Serikali kuokoa timu za Gor, Starlets

Na MHARIRI

BAADA ya maji kuzidi unga katika masuala ya ufadhili wa timu za Harambee Starlets na Gor Mahia zilijipata katika kona mbaya na hivyo kukodolewa macho na uwezekano wa kukosa kushiriki michuano ya kimataifa wikendi hii.

Mwanzo, timu ya taifa ya akina dada ya Harambee Starlets ililazimika kuvunja kambi yake siku ya Jumanne wiki hii kutokana na ukosefu wa hela za kuwadumisha mabinti hawa kambini walipokuwa wanajiandaa kuchuana na wenzao wa Zambia katika mchujo wa ngarambe ya kuwania kufuzu kwa michuano ya Olimpiki ya Tokyo itakayofanyika mwaka wa 2020. Mkondo wa kwanza wa mchuano huu unachezwa wikendi hii katika uwanja wa Kimataifa wa Moi Kasarani.

Kwa upande mwingine, tangu SportPesa ilipoondoa ufadhili wake kwa klabu ya Gor Mahia kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa KPL mwaka huu, timu hii imejipata katika hali ngumu ya kifedha.

Timu hii imekuwa ikitegemea michango ya wasamaria wema kuendesha shughuli zake. Inapohitajika kusafairi kutoka nje ya nchi kwa michuano ya kimataifa, K’Ogalo imekuwa ikilazimika kuandaa michango ya harambee ili kujikwamua.

Kutokana na hali hii inazokumba timu hizi mbili, ilitarajiwa kwamba zilikuwa katika hatari ya kukosa kushiriki michuano ya kimataifa iwapo mfadhili au mhisani asingejitokeza kuzinusuru.

Changamoto hii ilimfanya rais wa Shirikisho la Soka nchini Nick Mwendwa kuanza kulumbana na Katibu katika wizara ya michezo Kirimi Kaberia kwa madai kwamba wizara ya michezo imedinda kutoa hela za ufadhili wa michezo licha ya kuwa na kitita kikubwa cha hela zilizotokana na ushuru ambao umekuwa ukitozwa kampuni za kamari nchini.

Mgalla muue na haki umpe. Kukerwa kwa Mwendwa kuna mashiko kwa sababu serikali imechangia pakubwa katika kuvuruga udhamini wa michezo nchini kuanzia mwaka huu.

Hatimaye, malumbano ya Mwendwa na Katibu katika Wizara ya Michezo yalizaa matunda. Gor Mahia ilinunuliwa tiketi za usafiri wa ndege kuelekea DR Congo kwa mechi ya marudiano dhidi ya klabu ya Motema Pembe katika kipute cha Kombe la Mashirikisho ya Soka Afrika nayo timu ya akina dada ya Harambee Starlets iliwezeshwa kurejelea mazoezi kujiandaa kwa mechi dhidi ya vipusa wa Zambia.

Hata hivyo, ni kosa serikali kusubiri kupapurwa kabla ya kuwajibika. Ni jukumu la serikali kufaa spoti nchini kupitia kwa ufadhili.

You can share this post!

Oparanya akashifu wakaguzi wa vitabu vya fedha

Maafisa zaidi ya 20 wakamatwa, wengine kadha wasakwa na...

adminleo