TAHARIRI: Jamii isiwawekee wanaume shinikizo
Na MHARIRI
VIONGOZI wanaume Jumatatu waliandaa kongamano kubwa katika mji wa Eldoret ambapo walijadili masuala yanayowahusu.
Kongamano hilo ambapo washiriki walitakiwa kulipa ada ya Sh2,000 mlangoni, lilivutia idadi kubwa ya wanaume, bila kujali gharama, ishara tosha kuwa walihitaji mno mafunzo.
Kwenye kongamano hilo, mada kadhaa zilijadiliwa, kubwa zaidi ikiwa kuhusiana na jinsi gani vijana wa sasa wanaweza kuwa ‘wanaume kamili’.
Jambo hili, kwa muda mrefu limekuwa likiwapiga chenga wanaume hapa Kenya, ambapo wengi wamebaki kuvumilia dhiki mikononi mwa wake zao au wapenzi, ambao sheria na jamii kwa jumla imekuwa ikiwachukulia kuwa wanaodhulumiwa.
Kutokana na jamii yetu kuwafunza wanaume kuwa watu wasiotarajiwa kuonyesha hadharani udhaifu wowote, vijana na wanaume wengi wameishia kuvumilia na kunyamaza wanapoteseka katika maisha ya ndoa.
Yaani mwanamume anatarajiwa na jamii kunyamaza kimya anapokumbwa na matatizo ya kiafya, kiuchumi na hata kijamii, ikisemekana kuwa kutangaza hadharani ni udhaifu.
Kwa sababu hiyo, kuna wanaume wengi wanaoumia kimyakimya ndani ya majumba yao.
Wengi ni wale wanaoamua kuingilia uraibu wa mihadarati na ulevi wa kupindukia, wakiamini ni mojawapo ya njia bora za kujiepusha na matatizo wanayopitia.
Isitoshe, sera nyingi za serikali zimeonekana kuzingatia zaidi maslahi ya wanwake na watoto wa kike.
Kwa mfano, japokuwa ni kweli kuwa wasichana wengi kutoka maeneo ya mashinani wanakumbwa na matatizo ya kukosa visodo na mahitaji mengine ya wasichana, hakuna juhudi sawa na hizo za kushughulikia matatizo wanayopata watoto wa kiume.
Na hata matatizo yao yanapoangaziwa, kama vile kujiingiza katika biashara za bodaboda au kuuza moguka, serikali huwachukulia kuwa wahalifu na kuwakanya kwa kutishia kuwakamata.
Mtoto wa kiume amesahauliwa katika mipango mingi ya Serikali, ambapo hata kwenye sera kama za Fedha za Vijana, msisitizo huwa kwa vijana wa kike.
Mipangilio hii inayotilia mkazo upande mmoja wa jinsia, huenda ni kati ya sababu zinazosababisha ongezeko la visa vya wanaume kujiua.
Ipo haja kwa serikali na jamii kwa jumla, kuwachukulia wanaume kuwa binadamu wa kawaida, badala ya kuwawekea shinikizo na matarajio yaliyo nje ya uwezo wao kama binadamu.