Makala

TAHARIRI: Jopokazi la BBI liongoze mikutano

January 29th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MHARIRI

MALUMBANO makali yanayoendelea baina ya wanasiasa wanaomuunga mkono Naibu Rais William Ruto na kinara wa upinzani, Raila Odinga, kuhusu ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI) yanapasa kusitishwa, na viongozi hao kushughulikia maswala yanayowaathiri raia wa kawaida.

Ilivyo ni kwamba, wanasiasa wa mirengo yote miwili wamezama kwenye siasa za kuvumisha vinara wao kama kwamba, uchaguzi mkuu wa 2022 utaandaliwa mwezi ujao. Hilo halifai kuruhusiwa kuendelea. Muafaka wa maridhiano kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga ulilenga kukuza uwiano na kuleta utangamano wa kitaifa. Hivyo basi, ripoti ya jopokazi hilo haifai kutumika kuvuruga amani na utulivu ambao umekuwepo tangu mahasimu hao wawili wa kisiasa wakumbatiane.

Inashangaza kwamba, licha ya washirika wa Bw Ruto na Bw Odinga kuafikiana kwa kauli moja kwamba, ripoti hiyo ina vipengee mbalimbali ambavyo vitaipeleka nchi mbele, bado kuna vuta nikuvute kuhusu utekelezaji wake.

Tunatoa wito kwa wanasiasa wa mirengo mbalimbali ya kisiasa nchini kuweka kando tofauti zao za kibinafsi na kwa mara ya kwanza, kuweka mbele maslahi ya nchi.

Mara kwa mara, Bw Odinga amesisitiza kuwa hajatangaza azima yake ya kuwania tena wadhifa wa urais ambao ameupigania mara nne. Wito wetu kwake na washirika wake ni kuhakikisha mikutano yote ya hadhara ambayo anandaa kwa jina la kuhamasisha umma kuhusu ripoti ya BBI haigezwi jukwaa la kumvumisha kisiasa na kuumbua wapinzani wake wa kisiasa.

Wakati huo huo, tunamhimiza Naibu Rais William Ruto kukumbuka kwamba, angali msaidizi wa Rais na hivyo hastahili kuchukua misimamo inayoonekana kukinzana na ile ya mkubwa wake. Hii ni kwa sababu, Bw Odinga kwa sasa aonekana kama kwamba anatumia vikao vya BBI kuendesha kampeni za 2022. Kwa upande wa pili, Bw Ruto ameamua kumkaidi rais na matokeo yake ni kupanda kwa joto la kisiasa kote nchini.

Wakati umewadia kwa wanachama wa jopokazi la BBI kujitenga na mikutano ya kisiasa inayoendeshwa kwa jina lake, kutoa ratiba rasmi ya vikao vya kuhamasisha Wakenya wa kawaida kisha kujumuisha mapendekezo yao kwenye ripoti ya mwisho. Ni kwa njia hiyo ambapo hatua ya wanasiasa kuteka mchakato wa mageuzi ya kikatiba inaweza kusitishwa.