TAHARIRI: Kazi kwa mahakama sasa kuhukumu mafisadi
NA MHARIRI
Kushtakiwa kwa Waziri wa Fedha Henry Rotich, Katibu wa Wizara Kamau Thugge na maafisa wakuu wengine wa Mamlaka ya Maendeleo ya Bonde la Kerio (KVDA) kuhusiana na sakata ya ufujaji wa Sh21 bilioni za mabwawa ya Kimawarer na Arror, kumedhihirisha kwamba hatimaye serikali imejitolea kukabiliana na ufisadi.
Iwapo upande wa mashtaka utafanikiwa kuwasilisha ushahidi wa kutosha kuthibitisha kuwa washukiwa walihusika na sakata hiyo, basi Kenya itakuwa imepiga hatua kubwa katika vita dhidi ya zimwi la ufisadi.
Tangu Rais Uhuru Kenyatta kutangaza vita dhidi ya ufisadi, mwaka mmoja uliopita, Wakenya hawajaona afisa wa ngazi ya juu serikalini akiadhibiwa mahakamani. Tunachoona ni mrundiko wa kesi za ufisadi mahakamani.
Mnamo Februari, Jaji Mkuu David Maraga alikutana na majaji na kutangaza kwamba Idara ya Mahakama imeweka mikakati kuhakikisha kesi za ufisadi zinasikizwa na kuamuliwa ndani ya miezi mitano.
Miongoni mwa mikakati ilikuwa kuongeza saa za kusikiza kesi za ufisadi. Ni wajibu wa Idara ya Mahakama kuhakikisha kwamba, mikakati hiyo iliyotangazwa miezi mitano iliyopita inatekelezwa.
Jaji Maraga alishutumu afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuwa inahusika katika ucheleweshaji wa kesi kwa kuwasilisha ushahidi usioafiki viwango vinavyohitajika.
Afisi ya DPP haina budi kuhakikisha inawasilisha ushahidi wa kutosha ili kesi hizo zikamilishwe upesi.
Serikali imetumia mabilioni ya fedha kufadhili Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC), afisi ya DPP, Idara ya Uchunguzi wa Uhalifu (DCI), Mamlaka ya Kurejesha Mali ya Umma (UARA), Kituo cha Kupokea Ripoti za Uhalifu wa Fedha.
Wakenya wanataka kuona wahusika wa sakata kubwa za ufisadi wakiadhibiwa na kutwaa mali ya umma iliyonyakuliwa kiharamu.
Wanasiasa nao wakome kuingiza siasa katika vita dhidi ya ufisadi.
Tayari baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakitumia mitandao ya kijamii kueneza chuki kwamba kukamatwa kwa Waziri Rotich kunatokana na siasa za 2022.
Kauli za aina hiyo zimekuwa changamoto kubwa katika kupambana na wizi wa fedha za umma nchini kwa miaka mingi.
Serikali haina budi kuwakabili wanasiasa hawa ambao huenda wakachochea uhasama wa kikabila nchini.
Hatutaweza kushinda vita dhidi ya ufisadi ikiwa Wakenya watagawanyika kwa misingi ya vyama vya kisiasa au kabila.
Hatutaweza kushinda vita dhidi ya ufisadi ikiwa Wakenya watagawanyika kwa misingi ya vyama vya kisiasa au kabila.