TAHARIRI: Kazi Mtaani itimize malengo ya serikali
Na MHARIRI
JANGA la corona lilipotangazwa kuingia humu nchini, watu binafsi na hata mashirika yaliathirika vibaya kiuchumi.
Hata kufikia leo Ijumaa, kuna maelfu ya watu wanaoendelea kufanya kazi wakiwa nyumbani.
Zaidi ya watu milioni moja tayari wamefutwa kazi, wengi wakiwa katika sekta za utalii, kilimo, mawasiliano na elimu. Kwa mfano maelfu ya walikuwa walioajiriwa katika shule za kibinafsi hawana kazi, na wala hakuna uhakika kwamba shule zitakapofunguliwa, watapata ajira.
Katika mahangaiko haya, walioathirika zaidi ni vijana wa vyuo anuai na vikuu ambao walirejea nyumbani kwao wakiwa hawana jambo la kuwashughulisha.
Ikizingatiwa kuwa asiye na la kufanya ni mwepesi wa kushawishiwa kujiunga na maovu, ilikuwa wazi kwamba wangeathirika kimaadili.
Kuna maelfu ya vijana waliokuwa na biashara zilizoathiriwa na ujio wa Covid-19, jambo lililoilazimu serikali kuja na mradi wa kusafisha mitaa ‘Kazi Mtaani’.
Serikali ilikuwa na nia njema, hasa ilipoamua kupunguza malipo ya kila siku kutoka Sh600 hadi 450 ili kutoa nafasi ya vijana wengi zaidi kuingia kwenye mpango huo.
Lakini tangu mpango huo uanze karibu miezi mitatu iliyopita, hakujaonekana mabadiliko yoyote ya kimazingira katika maeneo mengi nchini.
Katika jiji la Nairobi, vijana hushughulika na kazi moja siku nenda siku rudi, huku shughuli muhimu za usafi kama kuzoa taka au kuziba mashimo zikiendelea kufanywa na wafanyikazi wa kaunti.
Sababu ya kuanzisha mradi huo ilikuwa ya kuwapa vijana mapato, lakini kwa vile wanalipwa pesa za mlipa ushuru, ni lazima wazitolee jasho. Imebainika kwamba katika maeneo mengi ya nchi, vijana hujishughulisha tu na kusafisha mabomba ya majitaka kila siku. Wengine kazi yao ni kufyeka eneo moja hata kama nyasi hazijamea. Kuna wale wanaoshirikiana na vijana wa NYS kufika kazini, kutia saini na kwenda zao.
Kufanya mradi huu bila ya kuzingatia manufaa yake kwa mwananchi, ni kutumia vibaya pesa za umma. Kwa nini kwa mfano kusiwe na ratiba maalumu ya shughuli za kufanywa kila siku? Mbona wizara inayohusika na vijana isiwateue kutokana na ujuzi walio nao?
Kama serikali kweli inataka kukabili ukosefu wa ajira, basi yafaa mradiu huu upigwe msasa kama wanavyopendekeza wabunge.