TAHARIRI: Korti ziongezewe pesa kuimarisha kazi
NA MHARIRI
KAULI ya Jaji Mkuu David Maraga, kwamba ukosefu wa majaji wa kutosha ndio umekuwa ukichelewesha baadhi ya kesi kuisha inapaswa kuchukuliwa kwa uzito.
Jaji Maraga alisema kuwa hilo ndilo limesababisha mrundiko wa kesi katika mahakama nyingi nchini, hali ambayo imezua mahangaiko mengi kwa wananchi.
Hili ni jambo linalopaswa kuiamsha Serikali Kuu, hasa Bunge la Kitaifa, kuhusu haja ya kuongeza mgao wa fedha kwa asasi hiyo muhimu, kwani imeibika kuwa tatizo hilo limechangiwa na ukosefu wa fedha za kutosha.
Kulingana na Bw Maraga, idara hiyo imepangiwa kupokea Sh17.5 bilioni kuendesha shughuli zake katika mwaka kifedha wa 2019/2020, licha ya kuomba kutengewa Sh32 bilioni.
Kimsingi, hii si mara ya kwanza kwa Jaji Mkuu kulalamikia tatizo hili. Mwaka uliopita, alilalama kuwa ilibidi idara hiyo kusimamisha baadhi ya miradi muhimu, baada ya Serikali Kuu kusambaratisha taratibu za ufadhili kutoka nje.
Ni kinaya kwa idara hii kulalamika kutopokea fedha, ikizingatiwa ni mojawapo ya matawi matatu makuu ya serikali.
Vile vile, ni sikitiko kuwa malalamishi haya yanajiri wakati Rais Uhuru Kenyatta ametangaza vita vikali dhidi ya wale wanaopatikana kushiriki katika sakata za ufisadi.
Katika hotuba zake kadhaa, Rais amelalamikia utendakazi wa idara hii, akisema kuwa baadhi ya kesi za washukiwa wakuu zinachelewa sana, hali ambayo inapunguza matumaini ya Wakenya kuhusu vita hivyo.
Hata hivyo, Bw Maraga amekuwa akijitokeza wazi, akilalama kuwa idara hiyo haipati uungwaji mkono ufaao kutoka kwa asasi zingine za serikali kama inavyohitajika.
Kimsingi, majibizano kama haya si yenye manufaa kwa mwananchi, kwani yanashusha imani yake kwa serikali.
Baada ya kupitishwa kwa katiba ya sasa mnamo 2010, mojawapo ya matumaini ambayo Wakenya walikuwa nayo ni mageuzi kamili katika idara hii, hasa uharakishaji wa kesi.
Kuna mageuzi kadhaa yanayoonekana wazi, kwani maafisa wa mahakama waliopo wamekuwa wakijaribu kuimarisha utendakazi wao.
Imefikia wakati idara hii inapaswa kufadhiliwa ifaavyo ili kuhakikisha kuwa utoaji haki unaharakishwa.
Malalamishi yake yanapaswa kuzingatiwa, ili kutoirejesha nchi wakati ambapo kesi zilikuwa zikichukua hadi miaka kumi kukamilika.