TAHARIRI: Kufuzu Afcon sio hoja, tujiandae kwa mtihani kamili
NA MHARIRI
KWANZA ni pongezi kwa eneo la Afrika Mashariki kwa kuingiza timu nne katika fainali za Mashindano ya Kombe la Afrika (AFCON). Kwa mara ya kwanza katika kipindi cha muda mrefu, mwezi Juni na Julai raia wa Kenya, Uganda, Tanzania na Burundi hawatakuwa wakimeza mate kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Kenya ndiyo ya majuzi zaidi kushiriki mashindano hayo mwaka 2004 nchini Tunisia. Tanzania ilishiriki mwaka 1980, Uganda mwaka 1978 ilhali Burundi inaingia mashindano hayo kwa mara ya kwanza.
Kenya haikufanya vyema miaka 15 iliyopita, ilipokuwa chini ya mkufunzi Jacob Ghost Mulee. Safari hii, timu yetu ya taifa Harambee Stars angalau ina wachezaji wa kimataifa kama vile Victor Wanyama, Michael Olunga kati yaw engine, ambao wamepata uzoefu wa mechi za kimataifa.
Japokuwa Harambee Stars ina wachezaji wenye hadhi, tatizo letu kila mwaka limekuwa jinsi ya kuwajali kimaslahi.
Mchezaji kama Wanyama, analipwa mshahara wa Pauni 70,000 (Sh9.3 milioni) kwa wiki, huenda hataichezea Harambee Stars kwa kutarajia mshahara. Lakini Shirikisho la Soka nchini (FKF) na serikali kupitia wizara ya Michezo, angalau wanapaswa kumpa hadhi anayostahili.
Wenzake wa humu nchini pia wana haki zao za kimsingi zinazofaa kuangaliwa. Wachezaji wetu wamekuwa wakiachwa kwenye vyumba vichafu vya hoteli, bila mlo mzuri na hata marupurupu kidogo.
Maafisa wa serikali wanaoandamana na timu wamekuwa na mtindo wa kuwachukua wapenzi wao, na kutumia pesa za serikali katika anasa huku wachezaji na wakuu wa timu wakiteseka.
Wakati wa fainali za Kombe la Dunia nchini Urusi, wabunge walienda huko na kupoteza pesa za mlipa ushuru bila kuwa na mchango wowote. Ni matumaini yetu kuwa hakutakuwa na ujumbe mkubwa wa wanasiasa na marafiki zao kuliko wachezaji.
Hali hii isipobadilika, tusitarajie makubwa katika mashindano ya nchini Misri.Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), Nicholas Musonye, ana kibaria cha kushawishi mataifa yote manne yakitolee kudhamini timu zao.
Nchi zilizoimarika katika mchezo wa kandanda, serikali zao huwekeza pakubwa kuhakikisha wachezaji hawalii ngoa.
Tusipofanya hivyo, tutarejelea tatizo lile lile la kuwa wasindikizaji, huku wenzetu wa Afrika Kaskazini, Kusini na Magharibi wakisonga kutoka hatua ya makundi.