• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 4:23 PM
TAHARIRI: Lazima tumuunge mkono Rais kukabili ufisadi

TAHARIRI: Lazima tumuunge mkono Rais kukabili ufisadi

Na MHARIRI

KAULI ya Rais Uhuru Kenyatta Jumapili kwamba kila Mkenya anapaswa kujiunga naye kwenye vita dhidi ya ufisadi inapaswa kuungwa mkono na kila mmoja wetu.

Tamko la rais kwamba vita hivyo vimemfanya hata kupoteza baadhi ya marafiki wake wa karibu, ni ishara ya wazi kwamba kinyume na ilivyokuwa awali, amejitolea kikamilifu kubadili mkondo ambapo watu wamekuwa wakikwepa sheria, hata inapobainika kuwa wamefuja fedha za umma.

Ni dhahiri kuwa tangu uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka (DPP) Noordin Haji, Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi George Kinoti mapema mwaka huu, mwelekeo dhidi ya ufisadi umebadilika nchini.

Kwa ushirikiano na Tume ya Maadili na Kukabiliana na Ufisadi (EACC), wawili hao wamefufua matumaini ya Wakenya kwamba inawezekana kwa janga hilo kukabiliwa, hasa miongoni mwa watu wenye ushawishi.

Kwa wito wake jana, rais anaonyesha nia ya kuikomboa Kenya kutoka minyororo ya ufisadi, ambayo imeigeuza mateka kwa karibu miongo mitano kufikia sasa.

Kiini cha Wakenya wengi kupoteza imani na vita dhidi ya ufisadi ni kwamba juhudi zote za hapo awali hazijazaa matunda hata kidogo.

Kwa mfano, vita na msisimko mpya wa mapambazuko ya kiutawala ulioshuhudiwa Kenya mnamo 2003 haukudumu kwa muda mrefu.

Baada ya kuapishwa, Rais Mstaafu Mwai Kibaki alitangaza wazi kwamba ufisadi ungekuwa jambo la kwanza kulikabili, ili kulainisha utoaji huduma kwa wananchi na idara mbalimbali za serikali.

Kwa matumaini makubwa, Wakenya walikumbatia kauli yake kwa ukunjufu na matumaini makubwa sana. Hata hivyo, matumaini yap yalianza kudidimia baada ya sakata za ufisadi kuwaandama baadhi ya mawaziri waliokuwa katika serikali yake.

Baada ya muda, Kenya ilirudi pale pale ilivyokuwa. Saratani ya ufisadi ikatuandama tena.

Hata hivyo, matukio ya hivi karibuni ambapo maafisa wakuu serikalini wamekamatwa na kufikishwa mahakamani ni dalili za wazi kuwa Rais Kenyatta hajali matokeo ya kisiasa, ila lengo kuu ni kurejesha imani kuwa sheria haijatengenezwa kuwabagua maskini.

Wito wetu ni kwa wadau wote, kujiunga naye kuirejesha Kenya ilivyokusudiwa na mababu zetu wakati wa uhuru. Haifai kuketi na kutazama wafisadi wakila hongo, tukiamini ni jukumu la polisi pekee.

You can share this post!

OBARA: Kutunza mazingira ni bora kuliko ajenda zote

Apoteza demu kwa kimya cha siku mbili

adminleo