TAHARIRI: Maamuzi magumu yahitajika kuzima ufisadi
NA MHARIRI
Hatimaye Hotuba ya Rais kwa Taifa iliyosubiriwa na wengi ilifanyika Alhamisi na maoni mbalimbali yamemiminika kutoka pande nyingi.
Kuna zile pande haswa zinazohusisha viongozi serikalini na wanasiasa, ambao kauli zao ziliashiria kuridhika na hotuba hiyo.
Na kuna pande nyingine inayohusisha zaidi Wakenya wa kawaida ambao wengi wao walihisi kwamba Rais Uhuru Kenyatta alionekana mpole zaidi.
Ikiwa jumbe na maoni yao mengi kwenye mitandao ya kijamii ni ya kuaminika, ni wazi kwamba wengi wa Wakenya walitarajia Rais azungumze kwa ukali zaidi na haswa aonekane kufanya maamuzi bayana yanayomboresha mwananchi wa kawaida moja kwa moja.
Ukweli uliopo ni kwamba taifa hili halijawahi kupungukiwa na mawaidha na mapendekezo mazuri ya kupigisha taifa mbele.
Nchi ina Katiba ambayo iliwahi kusifiwa kuwa mojawapo ya bora zaidi duniani, na kinachokosekana wakati wote ni maafisa walio na uwezo, uaminifu na ujasiri wa kutenda kama inavyopendekeza Katiba.
Rais Kenyatta mwenyewe hajawahi kupungukiwa na maneno ya kutia moyo, kuonya, kuhakikishia umma na kuahidi kuchukua hatua kwa wale wanaokwenda kinyume na maagizo yake.
Takriban kila hotuba, Rais ameyazungumzia yote hayo kwa msisitizo mkubwa. Ila kile ambacho kimekuwa wazi ni kwamba inapokuja katika suala la utekelezaji, ugumu fulani unatokea.
Kwa hotuba ya jana Rais aliungama mwenyewe kwamba anafahamu yupo kwenye shinikizo nyingi kutimua maafisa wafisadi.
Na kumekuwa na tetesi za mara kwa mara kwamba ananuia kufuta maafisa wafisadi na kuunda upya baraza la mawaziri. Na ingawa alisema kwamba hatua ya kutimua wafisadi itaongozwa na sheria, ukweli ni kwamba hiyo kwa mara nyingine itatumiwa na baadhi kujificha na kukwepa kuchukuliwa hatua.
Malalamiko ya utendakazi duni ni mengi, sawa na ilivyo vilio kuhusu ufisadi. Mamilioni ya Wakenya wanasakamwa na ugumu wa maisha, itakuwa bora zaidi kwa Rais asikilize kilio cha wengi na kuchukua hatua zitakazorudisha imani ya umma katika utawala wa kisheria.