TAHARIRI: Mabadiliko ya kweli yaanze na viongozi
Na MHARIRI
WAKENYA wanapoadhimisha miaka 10 tangu kurasimishwa kwa Katiba mpya, kuna masuala kadhaa ambayo hayajatekelezwa.
Japo marekebisho yanayopigiwa upato hasa baada ya kubuniwa kwa jopokazi la Maridhiano (BBI) yanafaa, viongozi na wadau wote yafaa washirikiane kuhakikisha mabadiliko hayo yananufaisha raia na sio viongozi.
Ilipoidhinishwa siku kama ya leo mnamo 2010, Wakenya walikuwa na matumaini kwamba katiba ingeleta mabadiliko.
Hata hivyo, matarajio mengi hayajatimizwa, asa huku baadhi ya asasi zikipigania majukumu mbalimbali. Mabunge ya Seneti na Kitaifa yamekuwa yakizozana kuhusu ni bunge lipi lina mamlaka makubwa.
Utata huo mara nyingi hushuhudiwa wakati wa kupitishwa kwa sheria au upigaji msasa wa utendakazi wa mawaziri kati ya majukumu mengine ya kiserikali.
Hata baada ya makamishina wa Tume ya Uchaguzi kubadilishwa kila mara, upinzani haukuridhika na chaguzi za 2013 na zile mbili za 2017. Ghasia zilizuka na mauaji kutokea tu kama miaka ya nyuma. hii ikiwa dhibitisho tosha kwamba licha ya uwepo wa katiba hii,
Pia gurudumu la upatikanaji wa haki linakwenda kwa mwendo wa kinyonga hata baada ya idara ya mahakama kufanyiwa mageuzi mapya kwenye katiba ya sasa.
Mahakama na afisi za DPP, DCI na EACC zimekuwa zikilaumiana hasa kuhusu kesi za ufisadi.
Jaji Mkuu David Maraga amekuwa akidai kwamba kesi zinazowasilishwa hazina ushahidi wa kutosha kuwafungulia mashtaka washukiwa.
Kwa upande mwingine, DPP imekuwa ikidai korti inawaachilia washukiwa kwa dhamana ya chini na pia majukumu ya afisi hiyo ya Noordin Haji yamekuwa yakigongana na yale ya DCI.
Mswada wa Jinsia ambapo ungehakikisha wanawake wanatwaa theluthi mbili ya nyadhifa kwenye tume mbalimbali umekosa kupitishwa bungeni mara nne.
Hata hivyo, mfumo wa ugatuzi ambao ulianzishwa baada ya kupitishwa kwa Katiba mpya umeleta matunda mazuri na wakati huo huo kutoa nafasi kwa magavana kupora mali ya umma bila uoga. Ufanisi wa vita dhidi ya ufisadi bado ni ndoto.
Japo marekebisho yanayotajwa yanafaa, ni vyema iwapo yatatekelezwa na sio kupachikwa tu kama njia ya kuridhisha mrengo fulani wa kisiasa.