TAHARIRI: Madai ya kampuni za mahindi yamulikwe
NA MHARIRI
MADAI ya kampuni za kusaga unga wa mahindi kwamba bodi ya kusimamia Hifadhi ya maalumu ya Chakula (SFR) na Bodi ya Nafaka na Mazao nchini (NCPB) ziliruhusu usambazaji wa mahindi yenye sumu ya aflatoxin ambayo husababisha kansa hazifai kupuuzwa.
Ingawa wakuu wa mashirika hayo walikanusha madai hayo, sio mara ya kwanza kwa maafisa wa serikali au asasi za serikali kukataa njama zao zinapofichuliwa.
Ikizingatiwa kwamba kuna kampuni zilizosimamishwa kusaga unga ikisemekana una sumu, madai ya kampuni hizo yana uzito kwa sababu huwa zinanunua mahindi kutoka kwa Bodi ya Nafaka na Mazao.
Kampuni hizo zinadai kuwa SFR imekuwa ikizitaka zinunue mahindi yaliyo na sumu ya aflatoxin na wachanganye na mahindi safi kwa lengo la kuzuia uhaba wa chakula nchini.
Kulingana na kampuni hizo, maghala hayo yanahifadhi mahindi yaliyonunuliwa kutoka Uganda.
Haya ni madai ambayo hayawezi kupuuzwa ikizingatiwa kuwa mwaka jana, wakulima wa humu nchini walikosa kununuliwa mahindi yao huku wafanyabiashara walaghai wakishirikiana na maafisa wa bodi kununua mahindi kutoka nje ya nchi.
Ikiwa ni kweli bodi ililazimisha kampuni kuchanganya mahindi yenye sumu, basi inafaa kubeba lawama kwa kuhatarisha maisha ya Kenya.
Ni serikali iliyopiga marufuku unga wa kampuni kadhaa kwa madai kuwa hatari kwa afya kutokana na sumu. Ni masikitiko makuu kwamba badala ya kulinda raia, serikali inacheza shere na maisha yao.
Kwa upande mwingine, itakuwa makosa kwa kampuni hizo kutoa madai hayo kwa sababu ya kukaziwa masharti na serikali waweze kudumisha viwango vya ubora.
Mwenyekiti wa SFR Noah Wekesa, alisema kuchanganya mahindi yasiyofaa kuliwa na binadamu na mahindi safi ni kinyume cha sheria na wanaohusika wanafaa kuchunguzwa.
Bw Wekesa pia anafaa kuchunguza maafisa wa bodi yake badala ya kukanusha madai ya kampuni hizi bila ushahidi.
Ni makosa kucheza na afya ya Wakenya na suala hilo halifai kuchukuliwa kwa mzaha ili kulinda maslahi ya kibinafsi. Uchunguzi wa kina unapaswa kufanywa na shirika huru kubaini madai ya kampuni hizi na ikibainika ni ya kwali wahusika kuchukuliwa hatua.