Makala

TAHARIRI: Mashirika okoeni soka yetu isidorore

August 31st, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

MAPEMA Agosti 2019 mdhamini wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL), SportPesa alijiondoa katika ufadhili wa shindano hilo la mpira wa kandanda.

SportPesa ambayo hudhamini ligi hiyo kwa takriban Sh250 milioni kwa mwaka, ilichukua hatua hiyo baada ya biashara yake pamoja na ya kampuni nyinginezo za kamari ya michezo kupigwa marufuku kutokana na mgogoro wa ushuru.

Serikali inadai kuwa kampuni hiyo maarufu pamoja na nyinginezo hazijalipa ushuru inavyofaa, nazo kampuni hizo hasiriwa zinasema zimelipa kodi hiyo kikamilifu kwa hivyo zinaonewa bure bilashi.

Lakini bila kujali ni yupi kati ya wahusika hawa anayesema ukweli, uhalisia uliopo ni kwamba, soka ya Kenya kwa ngazi ya kitaifa, haina mdhamini na hivyo inakabiliana na tatizo kubwa ambalo halijawahi kuonekana -ukosefu wa pesa.

Ligi Kuu ya Kenya (KPL) iling’oa nanga jana huku timu nyingi zinazoshiriki zikielezea wasiwasi wazo kuwa huenda zisifikie upeo wa mafanikio msimu huu kutokana na uhaba wa pesa.

AFC Leopards na Gor Mahia ambazo zimekuwa zikidhaminiwa na kampuni hiyo ya kamari ndizo zitakazopata pigo kubwa kwani zitapoteza takriban Sh50 milioni kila moja zinazotolewa na SportPesa kama ufadhili kwa mwaka.

Kinachozua taharuki hata zaidi ni kuwa, hamna anayejua ni lini ambapo mgogoro wa SportPesa na serikali utaisha ndipo udhamini huo urejelewe.

Kwa sababu hiyo, kama njia ya kujiokoa, klabu hizi mbili zimebuni njia mbadala za kujisaidia ambapo zimeunda mfumo wa simu utakaowezesha mashabiki kuzichangia.

Hata hivyo, kwa kurejelea historia, huenda mpango huo usifanikiwe inavyofaa.

Hivyo basi pana haja ya masharika mengine ya kibiashara pamoja na wahisani kujitokeza ili kuokoa timu hizi na ikiwezekana ligi kuu pia.

Japo mazingira ya kibiashara yameonekana kuwa magumu, ni muhimu wenye uwezo wazingatie tamathali “kutoa ni moyo usambe ni utajiri”.

Wengi wanatarajia kampuni zinazofana kwa sasa kama vile Safaricom, benki za KCB, Co-operative, Equity na nyinginezo zijitolee kuziba pengo hili linaloachwa na SportPesa ili kandanda yetu inusurike.

Kwa kufanya hivyo watakuwa wameokoa vijana wengi wanaoweza kuathirika na sintofahamu inayoendelea kukumba sekta ya michezo.