TAHARIRI: Mgomo utahujumu maandalizi shuleni
NA MHARIRI
TANGAZO la Katibu Mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Walimu nchini (KNUT) kwamba huenda kitaandaa mgomo wa kitaifa wa walimu iwapo Tume ya Kuwaajiri Walimu (TSC) haitasitisha mpango wake wa kuwahamisha walimu mbali na maeneo walikozaliwa ni usaliti mkubwa unaostahili kupingwa na Wakenya wote.
Kwanza, walimu, kama watumishi wowote wale wa umma waliafikiana na mwajiri wao kufanya kazi popote katika Jamhuri ya Kenya walipoajiriwa. Hivyo basi, ni jambo la kushangaza kwamba, viongozi wa walimu wanatishia kufanya maandamano kupinga sera ambayo, tunaamini, itawawezesha walimu kumakinika kazini kuliko ilivyo kwa sasa.
Ukweli mchungu ni kwamba, baadhi ya walimu, hasa wakuu wa shule, hutumia muda mfupi kufuatilia yanayoendelea shuleni mwao huku wakiendesha msururu wa biashara makwao. Isitoshe, wazazi wengi wamelazimika kuandamana na wengine hata kuvamia shule kulalamikia matokeo duni ya mitihani ya kitaifa baada ya kushuhudia uzembe wa wakuu hao wa shule mwaka mzima.
Pengine haya ni masuala ambayo Katibu Mkuu Wilson Sossion na wenzake katika makao makuu ya Knut jijini Nairobi hawayafahamu.
Ni haki ya kikatiba ya kila mmoja kupigania maslahi yake binafsi. Ama kweli hali hiyo ya ubinafsi ndiyo inatutofautisha na wanyama wengine.
Lakini ni hujuma kubwa kwa wakuu hao wa walimu kucheza karata na maisha ya maelfu ya wanafunzi katika shule za umma, hasa katika muhula huu ambapo wanajinoa tayari kwa mitihani ya kitaifa baadaye mwezi ujao.
Mbona wakuu hao hawakaripii wanachama wao wanaofika kazini walevi, wanaotoroka shule mapema, wanaoendesha biashara kwenye vituo vya kibiashara karibu na shule?
Mbona hawakemei walimu ambao ufahamu wao wa dhana za kimsingi, hasa katika somo la Hisabati ni sawa na ule wa wanafunzi wa shule za msingi?
Tunachosema hapa ni kwamba, wakati umefika kwa Knut kuwajibika sio tu kwa wanachama wake bali pia kwa wazazi wanaotumia maelfu ya pesa kuwaelimisha watoto wao. Sio haki kamwe, kwa walimu kutumia watoto wasio na hatia kama ngao kila wanapopigania haki na maslahi yao.
Vile vile, tungependa kutaja hapa kwamba, ni katika taaluma ya ualimu pekee ambapo, yamkini, mwajiri hana usemi wowote kuhusu masharti na kanuni za utendakazi.
Wafanyikazi katika taasisi zote za kibinafsi hupigwa msasa mara kwa mara huku utendakazi wao ukiwekwa kwenye mizani kila baada ya miezi sita. Hatua hiyo uhakikisha wahudumu wote wanajikakamua kazini na kuboresha uzalishaji wao. Mbona walimu wetu wasikubali mwajiri wao kupiga darubini utendakazi wao mara kwa mara?