Makala

TAHARIRI: Miguna hakustahili kudhalilishwa JKIA

March 28th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na MHARIRI

SERIKALI inapaswa kushughulikia utata kuhusu uraia wa mwanaharati wa upinzani Miguna Miguna kwa kufuata sheria bila kuwasha tena joto la kisiasa nchini.

Matukio yaliyoshuhudiwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta Jumatatu ni ya aibu, izingatiwa kuwa mahakama ilikuwa imetoa maagizo wazi kuhusu urejeo wa Miguna.

Haikufaa kwa serikali kumlazimisha Miguna kuingia ndege iliyoelekea Dubai, kwa sababu ya kukataa kupeana pasipoti yake.

Miguna si mgeni Kenya, jamaa na familia yake wanajulikana. Kwa hivyo ni bayana wakili huyo ni raia wa Kenya kwa kuzaliwa.

Hatusemi kuwa hakuna kasoro kuhusu stakabadhi za usafiri za Miguna, lakini dosari zilizopo zinaweza kurekebishwa bila sarakasi zinazoharibia Kenya sifa, hasa katika uwanja wa ndege wa kimataifa.

Ukweli mchungu ni kuwa, Wakenya walikuwa wamegawanyika katika makundi mawili katika uchaguzi uliopita na ni vyema tusifufue tena upepo huo. Nchi ilikuwa imeanza kutulia kisiasa baada ya Rais Uhuru Kenyatta na kinara wa upinzani Raila Odinga kusalimiana, lakini suala la Miguna linaturudisha hatua nyingi nyuma.

Miguna ni raia wakawaida na inashangaza jinsi serikali inamkabili kwa kutumia mamia ya GSU pamoja na jeshi ili kutatua suala dogo la uraia wake.

Bw Odinga alikuwa katika uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta kujaribu kumuokoa Miguna, na ilishangaza wengi kuwa wakili huyo alifurushwa hadi kwenye ndege bila yeye (Odinga) kusaidia chochote.

Muafaka aliyotia saini unampa nafasi ya kumpigia simu Rais Kenyatta na kutatua suala la Miguna bila sarakasi nyingi za kisiasa.

Muafaka wa viongozi hao wawili hautakuwa na maana iwapo raia wataendelea kushuhudia raia wa kawada wakihangaishwa na serikali ambayo inafaa kuwalinda. Kuungana kwao kwafaa kuunganisha Wakenya wote na wala si jamii au familia mbili.

Mahakama iliagiza Miguna aachiliwe na tunatarajia serikali itii maagizo ya korti ili suala la Miguna lisuluhishwe bila kuzua wasiwasi usiofaa.

Ikiwa kweli serikali inataka nchi hii kuendelea mbele, na serikali ifanikiwe katika nguzo zake nne za maendeleo ilizojiwekea, basi lazima kuwe na mandhari tulivu ya kisiasa.