TAHARIRI: Mikakati thabiti ya Simiyu itaokoa Shujaa
Na MHARIRI
KATIKA kipindi cha miaka 10 iliyopita ni makocha Innocent Simiyu na Benjamin Ayimba pekee ambao wamewahi kudhibiti mikoba ya timu ya taifa ya wanaraga saba kila upande, Shujaa, kwa zaidi ya misimu miwili.
Ayimba alishikilia wadhifa huo 2010-11 na pia 2015-16, naye Simiyu akapewa mikoba mara ya kwanza 2016-2018 na kisha Jumanne hii kwa mara ya pili. Simiyu, 37, aliteuliwa upya na Shirikisho la Raga la Kenya (KRU) mapema wiki hii kunoa timu ya taifa baada ya Paul Feeney wa New Zealand kugura mwezi Juni.
Uteuzi wake ulifanywa baada ya mchakato wa kipindi kirefu uliozingirwa na patashika za kila aina. Kazi hiyo ilivutia jumla ya wakufunzi 14, kati ya hao watatu wakiwa wa humu nchini – Simiyu, Paul Murunga na Dennis Mwanja, aliyeungwa mkono na idadi kubwa ya wanachama wa Bodi ya KRU.
Simiyu ana kibarua kigumu kurejesha umoja na ushirikiano miongoni mwa wadau wote wa raga humu nchini, na kuzima siasa nyingi zilizotawala uteuzi wake.
Hii ikizingatiwa kuwa idadi kubwa ya klabu za Ligi Kuu ya Kenya Cup, ambazo ndizo zitategemewa kuchangia wachezaji wa kikosi cha Shujaa, zilionekana kuegemea zaidi upande wa Mwanja anayeinoa klabu ya KCB.
Kati ya wanachama 15 wa Bodi ya KRU, tisa walimpigia kura Mwanja, watatu wakamuunga Simiyu na watatu wengine wakasusia zoezi hilo.
Simiyu atakuwa pia na kazi kubwa ya kurejesha imani ya wadau hasa kufuatia tukio la 2018 jijini Paris, Ufaransa. Wakati huo, wakiwa chini ya Simiyu, wanaraga wa Shujaa walilalamikia kutolipwa marupurupu kwa kuziba nembo ya Kenya na mdhamini (Wizara ya Utalii) kwenye jezi zao.
Simiyu ataanza rasmi kazi Oktoba kwa mkataba wa miaka miwili akitarajiwa kuongoza timu ya taifa kwenye Olimpiki zijazo jijini Tokyo, Japan, na mechi za kufuzu kwa Kombe la Dunia 2022 jijini Cape Town, Afrika Kusini.
Ipo haja kwa kocha huyo pamoja na KRU kubuni mikakati kabambe kuhakikisha kuwa wadau wa raga wanashirikiana kuirejesha Shujaa katika fahari yake ya hapo awali.
Mbali na kushughulikia malipo ya wachezaji mapema, italazimu Simiyu kuhakikisha kwamba uongozi wake haupuuzi wadau muhimu ikiwemo Kenya Cup, na ikiwezekana ashirikiane na Mwanja.
Kikosi cha Kenya kikifanya vizuri, kitavutia wadhamini mbalimbali ikiwemo Safaricom na Kenya Airways waliowahi kufadhili Shujaa katika kampeni za raga ya kimataifa.
Simiyu ni kocha mwenye ujuzi na tajriba kubwa kikosini Shujaa, itakuwa bora akiteua benchi nzuri ya kiufundi na kudumisha uhusiano mwema na vikosi vya Kenya Cup ili apate wanaraga wazoefu watakaotambisha timu ya taifa.
Mikakati thabiti ikibuniwa, Kenya itainuka na kujiondoa kwenye fedheha ambayo imekuwa ikikabiliana nayo katika miaka ya nyuma kweye ulingo wa raga.
Hata mkufunzi Paul Treu, aliyeongoza Afrika Kusini kutwaa taji la Raga ya Dunia 2009 na shaba katika Michezo ya Jumuiya ya Madola 2010, hakufaulu.
Kocha huyo mzawa wa Afrika Kusini alipokezwa mikoba ya Shujaa mnamo 2014.