TAHARIRI: Mikutano ya kisiasa heri iwe marufuku
KITENGO CHA UHARIRI
TAKWIMU zilizotolewa na Wizara ya Afya katika wiki moja iliyopita zinahofisa kwa kuweka rekodi ya idadi kubwa zaidi ya vifo vya waathiriwa wa corona kuwahi kupatikana tangu janga hili litue humu nchini.
Ripoti za Jumanne kwamba wanafunzi 52 katika shule moja pamoja na walumu sita na wafanyakazi wawili kupatikana na corona ni za kuhofisha.
Kufikia Jumatatu zaidi ya mia walikuwa wameuawa na Covid-19 ndani ya wiki moja. Tayari waliokuwa wamepoteza maisha yao kutokana na corona kwa jumla ni 1,027.
Bali na waliopoteza maisha yao, idadi ya maambukizi ya Covid-19 imepaa zaidi kiasi kwamba wataalamu wameanza kukisia kwamba huenda hizi ni dalili za mkumbo wa pili wa maambukizi haya hatari kuanza kushika kasi.
Wataalamu pia wameelezea sababu ya janga hili kukithiri ni kutokana na wananchi kutowajibika hasa kutozingatia maagizo ya serikali ya kuzima maambukizi ya gonjwa hili.
Maagizo haya yaliyopuuzwa ni kama kuvaa maski na kwa njia ifaayo, kuzingatia umbali wa mita na nusu pamoja na kunawa mikono ipasavyo. Mambo yalikwenda segemnege wakati kafyu ililegezwa, vilabu kufunguliwa huku ibada, harusi na mazishi yakirejelewa kama kawaida.
Suala la mapuuza limedhihirika wazi wazi kwenye mikutano ya kisiasa ambapo viongozi huwakusanya wananchi bila kujali uzingatiaji wa kanuni hizi za Wizara ya Afya.
Baadhi ya viongozi wameonekana wakitoa mifano mibovu ya kutovalia maski na hata kutowashauri wafuasi wao kuzingatia maagizo hayo. Suala hili limeghadhabisha viongozi wa kidini na wa wizara ambao wametoa wito mikutano yote hasa ya kisiasa nchini izimwe kote nchini ili kunusuru hali iliyopo kwa sasa.
Hata ingawa hali ya siasa nchini imechochewa na uzinduzi wa ripoti wa Mpango wa Maridhiano (BBI) ambayo kampeni zake zimeanza kwa kasi, serikali inafaa kufanya maamuzi ya busara kati ya siasa na thamani ya uhai wa raia wake.
Rais Uhuru Kenya anapojiandaa kutoa mwelekeo kuhusu mbinu mwafaka za kukomesha usambaaji wa homa hii hatari, anafaa kulipa kipaumbele suala la mikutano ya kisiasa ambayo inafaa kuzimwa kabisa kando na mbinu zingine faafu kukomesha janga hili linalokondolea macho maisha ya Wakenya.