• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 5:55 AM
TAHARIRI: Mizozo ya bajeti kauntini ikome

TAHARIRI: Mizozo ya bajeti kauntini ikome

NA MHARIRI

KUMEKUWA na matukio mengi ya mizozo kati ya madiwani na magavana kuhusu bajeti za serikali za kaunti mbalimbali.

Katika baadhi ya matukio hayo, ikiwemo ya majuzi zaidi katika Kaunti ya Taita Taveta, mvutano hutishia kusambaratisha utawala wote wa kaunti.

Viongozi katika kaunti zote wanahitajika kukumbatia mashauriano kutatua tofauti kati yao ili kuepusha madhara kwa wananchi.

Wakati mwingi, mizozo hii huwa haihusu hata maslahi ya wananchi bali ya viongozi wenyewe wanaojitafutia makuu.

Utakuta kwamba, madiwani wanafahamu fika bajeti wanayotaka iongezwe haiwezekani kuongezwa bila kudhuru shughuli za kaunti lakini bado watashikilia msimamo wao mkali wa kukataa kupitisha ile iliyopendekezwa na afisi ya gavana.

Wakati baadhi yao wakitaka kutengewa pesa zaidi wanazodai ni za kuimarisha maendeleo katika wadi wanazosimamia, kuna wale wasio na aibu ya kutaka mabunge yao yaongezwe fedha za matumizi.

Aibu ni kwamba, fedha hizo mara nyingi huwa hazitumiwi kwa manufaa yoyote ya umma bali kwa manufaa ya madiwani katika mambo kama vile kufadhili safari tele zisizo na maana, kulipia marupurupu ya burudani na mengineyo.

Viongozi wote wanahitaji kufahamu walichaguliwa kuwakilisha umma na hivyo basi yale yote wanayoyafanya yanafaa kuweka mbele maslahi ya umma.

Hili ni jambo ambalo hatutachoka kusisitiza hadi pale wanaoingiza ulafi katika uongozi wao watakapokoma au kukomeshwa.

Inasikitisha kuona shughuli za kaunti zikikwama kwa sababu ya ulafi wa madiwani au uchoyo wa gavana.

Kwa msingi huu, vitengo hivyo viwili vinafaa viwe vikishirikiana wakati wote kwa manufaa ya umma.

Viongozi hao wakumbuke kwamba hawatakuwa uongozini milele na hivyo basi wanapohujumu maendeleo, wanajiandalia maisha magumu hapo mbeleni.

Hitaji la kuleta maendeleo mashinani ni kwa manufaa ya kila mmoja wakiwemo wao wenyewe na jamii zao ambazo wanapokuwa mamlakani wanaona wako starehe.

Viongozi waweke ulafi wao kando, wawe wenye busara na wanaoweza kushirikiana katika kila jambo ili Kenya isonge mbele.

You can share this post!

Huyu Mbappe atavunja rekodi zote za Messi na Ronaldo

Ukahaba ni hatia kama uavyaji mimba – Serikali

adminleo