TAHARIRI: Ni mapema kufikiri kuzifungua shule
Na MHARIRI
WAZIRI wa Elimu, Profesa George Magoha mnamo Jumatano alitangaza kuwa kila darasa litahitajika kuwa na kati ya wanafunzi 15-20 shule zitakapofunguliwa Septemba.
Alisema wizara yake imeshauriwa kufanya hivyo kama njia mojawapo ya kuzuia kuenea kwa maambukizi ya virusi vya corona.
Ingawa hatua ya serikali kufungua shule ni nzuri, hakuna madarasa ya kutosha kukidhi hitaji hilo.
Sasa hivi, baadhi ya shule za umma zina hadi wanafunzi 70 kwa darasa. Je, hao wengine watasomea wapi?
Je, serikali ina uwezo wa kujenga madarasa ya ziada katika shule zote za umma kat ya sasa na Septemba? Na hata ikiweza, tatizo la uhaba wa walimu halijatatuliwa. Itakuwa vigumu na kazi kubwa kwa walimu hawa kufundisha somo moja kwa wanafunzi 15 tena kuyarudia mafunzo yayo hayo kwa wanafunzi wengine.
Kwa kifupi mpango wa wanafunzi 15 au 20 kwa kila darasa haliwezekani nchini na serikali inafaa kuibuka na mbinu nyingine kuhakikisha masomo yanaendelea kama zamani.
Katika kuzuia maambukizi zaidi serikali imetangaza kwamba itampa kila mwanafunzi barakoa mbili na pia kuwataka kuhakikisha usafi kwa kunawa mikono kila mara.
Hata hivyo, baadhi ya shule hasa zile za mashinani na maeneo kame hazina maji karibu. Je hawa watadumisha usafi kivipi?
Itawalazimu kubeba maji kutoka nyumbani tabia ambayo inaweza kupuuzwa kwa urahisi na baadhi yao.
Changamoto nyingine ni jinsi walimu watahakikisha wanafunzi wanazingatia hitaji la kuketi umbali wa mita moja unusu.
Wizara ya Afya pia, ilisema idadi ya maambukizi itakuwa ikifikia kilele chake Agosti au Septemba huku baadhi ya shule nazo zimekuwa zikitumika kuwatenga wanaopatikana na virusi hivyo.
Hii inamaanisha kwamba wagonjwa wengi watajitenga nyumbani shule zikifunguliwa. Hali hii itakuwa hatari na huenda ikapandisha maambukizi ya corona tena nchini.
Wanafunzi wa madarasa ya chekechea na mengine hawana ufahamu wa kina kuhusu virusi vya corona na hata iwapo wanao, watacheza na kutagusana shuleni kama zamani bila kuhofia athari ya virusi hivi.
Aidha janga la mafuriko lilisomba na kuharibu miundomsingi katika shule kadhaa, wanafunzi kutoka maeneo haya watasoma kivipi kwa kuzingatia masharti ya kuzuia kuenea kwa corona?
Hii ndiyo maana serikali inafaa kutathmini hali kwa mara nyingine kabla ya kufungua shule nchini.