TAHARIRI: Ni mapema mno kututwika mzigo
KITENGO CHA UHARIRI
ATHARI za janga la corona zinaendelea kuwakumba maelfu ya Wakenya, baadhi wakiwa hawajapata ajira tangu wapoteze vibarua katikati ya mwaka.
Sekta karibu zote za uchumi ziliathiriwa na kuja kwa ugonjwa huo. Jana, zaidi ya watu 500 walitangazwa kuwa walioambukiwa na maradhi hayo.
Serikali kupitia Rais Uhuru Kenyatta, iliweka mikakati kuwaondolea wananchi mzigo. Mipango hiyo ilihusisha kupunguzwa kwa ushuru wa mapato (PAYE), benki kutakiwa zijadiliane na wateja na kuangalia upya ulipaji mikopo, kutowaripoti watu kwa mashirika ya kukusanya habari za wasiolipa madeni (CRB), pamoja na kuagiza kampuni ya Safaricom isitoze ada usafirishaji pesa zisizozidi Sh1,000.
Afueni hiyo imekuwa muhimu sana kwa Wakenya, na kama wakipewa nafasi, wanaweza kutoa shukrani zao kwa serikali.
Ingawa sekta nyingi za kiuchumi zimeanza kufunguliwa upya, hali bado si nzuri. Wimbi la pili la Corona linaendelea kuua zaidi ya watu kumi kwa siku tangu mwezi Septemba. Hii ni ishara kuwa watu hawawezi kurejelea maisha ya kawaida mara moja bila ya kuchukua tahadharai.
Serikali imeendelea kuwataka wananchi wavae barakoa na kutekeleza masharti yote ya kudhibiti maambukizi ya Corona.
Utekelezaji huo pia ungefaa kuendelezwa kwa afueni waliypopewa wananchi. Lakini mambo ni tifauti kabisa. Taasisi mbalimbali za serikali zimeanza kuwarudishia mzigo wa gharama. Mamlaka ya Kudhibiti Kawi (EPRA) imekuwa mstari wa mbele kuwaongezea wateja bei ya mafuta kila mwezi. Sasa kuanzia Disemba 15 hadi Januari 14, wateja wa mafuta ya taa, dizeli na petroli watalipa bei ya juu. Hali hii imeendelea hivyo katika kipindi chote cha watu kukabiliana na janga hili la Covid-19.
Wizara ya Fedha imeshatangaza kwamba kufikia Januari, ushuru wa PAYE utaanza kurejea hali ya kawaida kwa watu wote wanapata Sh24,000 kwenda juu. Sasa Benki Kuu ya Kenya imeziruhusu benki zinanze kuwatoza wateja pesa kwa kusafirisha pesa. Agizo hili pia litahusu kampuni za kutoa huduma za pesa kwa simu.
Mzigo huo wa gharama ya maisha utaanza kutekelezwa wakati ambapo wazazi watatarajiwa kurejesha watoto wao shuleni, watakapokabiliwa na gharama mpya za kununua sanitaiza, barakoa, kulipa karo, kununua sare mpya na kadhalika. Huu bado si wakati bora wa kuwarudishia wananchi gharama.