TAHARIRI: NMS iangazie hii kero kwa wakazi
Na TAHARIRI
MNAMO Juni 28, 2020, Shirika la Huduma za eneo kuu la Nairobi Metropolitan (NMS) liliadhimisha siku 100 tangu liteuliwe kuwapa huduma wakazi wa Nairobi.
Rais Uhuru Kenyatta alimmiminia sifa Mkurugenzi Mkuu wa NMS, Meja Jenerali Mohamed Badi, kwa kuimarisha utoaji huduma.
Maagizo aliyokuwa ametoa Rais Kenyatta alipozindua NMS Machi 18, yalihusiana na kuimarisha ukusanyaji taka, huduma za maji na usafi, nyumba, ustawishaji jiji, uchukuzi na ujenzi wa barabara.
Kwa yeyote anayetembea katikati ya jiji, hatakosa kuona barabara zikiwa zimezibwa mashimo, zimechorwa mistari mieupe na ya manjano. Maeneo ya kuegesha magari yamechorwa vyema na mengine yamefungwa, kama njia ya kupunguza magari jijini. Hizi ni hatua nzuri ambazo NMS yapaswa kuziendeleza.
Wakati wa kumkabidhi Rais Kenyatta ripoti ya utekelezaji wa maagizo yake, Bw Badi alitangaza kwamba amekamilisha angalau asilimia 30 ya urekebishaji wa barabara zote.
Ingawa ni kweli kuwa hili limetimizwa katikati ya jiji, maeneo yanayopakana nayo yako katika hali mbovu sana. Mojawapo ya barabara ambazo zimetatiza wenye magari ni ile ya Muinami Street. Barabara hiyo ni muhimu sana kwa kuwa inaunganisha Hospitali ya Kujifungulia Kinamama ya Pumwani Maternity pamoja na ile ya kibinafsi ya Care Hospital.
Mgonjwa anapokimbizwa katika hospitali hizo mbili kutoka sehemu za Gikomba, Pumwani au Majengo, huchukua muda mrefu kutokana na kukatika kabisa kwa barabara hiyo eneo karibu na jumba la Mabruk.
Kadhalika, barabara nyingi zinazounganisha mitaa ya Eastleigh zimetelekezwa kwa muda mrefu, japo eneo hilo linatekeleza nafasi muhimu katika uchumi wa Nairobi na nchi nzima kwa jumla.
Tatizo jingine ambalo NMS na Meja Jenerali Badi wanapaswa kukabiliana nalo, ni lile la watu wanaojipa jukumu la kuegesha magari jijini. Watu hao maarufu kama ‘Parking Boys’ si tu kero kwa wamiliki wa magari ya kibinafsi, bali baadhi wanahusika na wizi wa vioo na vipuri vingine vya magari. Uchunguzi unaonyesha kuwa jamaa hao hushirikiana na maafisa wa jiji na sasa wale wanaovaa sare za KRA.
Pia, kuna pendekezo la MCAs wa Nairobi kuwa vituo vya matatu viondolewe katikati mwa jiji.
Hili ni jambo linalofaa kuetekelezwa kwa haraka, ili Nairobi iwe sawa na miji mingine mikuu ulimwenguni, ambako watu wana nafasi ya kutembea bila kero kutoka kwa magari ya usafiri wa umma.