TAHARIRI: NTSA ianze sasa kukabili vifo njiani
Na MHARIRI
MWAKA huu wa 2020 umeanza kwa vifo vya zaidi ya watu kumi kutokana na ajali za barabarani.
Watu watano walikufa kwenye barabara ya Eldama-Ravine kwenda Eldoret, wakiwa wanatoka kwenye sherehe ya kukaribisha mwaka mpya.
Jumatano mchana, watu wawili walikufa kwenye ajali katika barabara ya Kericho kwenda Litein. Polisi walisema katika ajali hiyo gari la Probox liligongana na pikipiki.
Katika ajali nyingine mwanamume alikufa baada ya kugongwa na gari eneo la Kianyaga, Kaunti ya Kirinyaga.
Huu si mwanzo mzuri kwa nchi ambayo ina idara na vitengo mbalimbali vya kukabiliana na ajali za barabarani. Takwimu za Mamlaka ya Usalama barabarabi (NTSA), zinaonyesha kuwa watu 3,396 waliaga dunia kwenye ajali za barabarani mwaka 2019.
Wiki moja kabla ya sherehe za Krismasi, Idara ya Polisi na NTSA walitoa kauli ya pamoja na kuahidi kuchukua hatua za kuzuia vifo vya watu barabarani.
Hatua hizo kwa kiwango kikubwa ziliangazia zaidi magari ya usafiri wa umma kuliko yake ya kibinafsi. Inaeleweka kuwa gari linalobeba abiria huwa na watu wasiopungua 15 wakati wowote na ajali inapotokea, bifo vinaweza kuwa vingi.
Lakini pia mtu mmoja mmoja wa gari la kibinafsi huweza kufanya idadi hiyo kuwa ya juu. Hata kifo cha mtu mmoja kutokana na kutozingatiwa kwa usalama barabarani ni hatia.
Kati ya mikakati saba ambayo idara hizo mbili zilikubaliana, hili la kufuatilia mwendo ambao magari huendeshwa pamoja na kuwakagua madereva mara kwa mara kuona kama wana afya au hali njema ya kuwaruhusu kuwa barabarani, vinaweza kusaidia mno kupunguza maafa.
Kubwa zaidi ni kampeni za elimu ya umma kuhusu usalama wa kila mtu ndani na kando ya barabara zetu. Tatizo kubwa linalosababisha kutokea kwa ajali barabarani, ni kutojali.
Madereva wengi huendesha magari kana kwamba barabara ni yao peke yao. Huwapita wenzao hata kwenye kona au wakati mwingine husimamisha magari ghafla punde wanapopita.
Lakini wapitanjia na waendeshaji wa pikipiki pia wanachangia ajali hizi. Watu wengi mijini huvuka barabara wakiwa wana-chat kwenye simu zao, bila kuangalia kushoto au kulia kabla ya kuvuka.
Haya yafaa yakabiliwe mapema kabla hayajaleta maafa zaidi.