TAHARIRI: Pawepo sheria ya kulinda majeruhi
Na MHARIRI
SHIRIKISHO la Soka Nchini (FKF) wiki hii limejipata kwenye malumbano makali na uongozi wa Gor Mahia kuhusu ni nani anayefaa kugharimia matibabu ya kiungo Philemon Otieno ambaye aliumia akichezea timu ya taifa Harambee Stars mnamo Agosti.
Kiungo huyo mbunifu alipata jeraha baya la goti pale Stars ilipokomolewa 4-1 kupitia kwa mikwaju ya penalti na Taifa Stars ya Tanzania katika mechi ya kufuzu kwa Ubingwa wa Afrika almaarufu CHAN 2020.
Huku Gor wakishikilia kwamba FKF lazima igharimie matibabu ya mchezaji wao anayeendelea kunyanyasika kutokana na jeraha hilo, shirikisho nalo linasema hilo ni jukumu la klabu, ikisema haina fedha mbali na kusema kwamba hakuna sheria inayoilazimisha kumtibu mwanasoka anayeumia akichezea timu ya taifa.
Hapa ndipo swali linaibuka, je, kwa nini wadau wa soka nchini hawajawahi kufikiria kutunga sheria hiyo ili hali kama ya Philemon inapozuka, basi pawepo utaratibu wa kufuatwa?
Hali hii pia huenda ikasababisha klabu za soka nchini hasa zile maarufu kama Gor na AFC Leopards kutowaruhusu wachezaji wao washiriki mechi za Harambee Stars kutokana na ukosefu wa sheria au mwongozo wa kuwapa matibabu kila mara wanapoumia.
Ingawa wachezaji wengi wanaoshiriki ligi maarufu barani Ulaya hupokea matibabu kutoka kwa klabu zao wanapopata jeraha hata wakichezea mataifa yao, ni vyema FKF isilinganishe hali hiyo na klabu za hapa nchini ambazo hata fedha za kulipa mishahara na marupurupu huwa hazipatikani kwa wakati.
Vilevile wanasoka wanafaa kuhamasishwa ili kuweka sehemu ya fedha wanazopata kama akiba ili wazitumie wakati hali kama hii inapozuka badala ya kusubiri hatima yao iamuliwe na mivutano kuhusu aliye na jukumu la kugharimia matibabu yao.
Miaka michache iliyopita, wanasoka walibuni chama cha kupigania maslahi yao. Je, chama hiki bado kinaendeleza shughuli zake?
Iwapo kipo, wanachama wake wanafaa kuwarai wanasoka wajiunge nacho na kuwasilisha mchango wao wa kila mwezi ndipo wapate pa kukimbilia wanapokumbana na masaibu kama haya ya Bw Philemon na wanusuru taaluma yao ya soka.
Jeraha lolote huwa ni hatari kwa taaluma ya soka ya mchezaji yeyote ndiyo maana FKF na Gor wanafaa kukoma kulaumiana na kutafuta njia za kumtibu sogora huyu ndipo apone na arejee kusakata kabumbu.