• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 8:55 PM
TAHARIRI: Pesa za umma zitumiwe vyema

TAHARIRI: Pesa za umma zitumiwe vyema

Na MHARIRI

SIKU chache baada ya makubaliano kupatikana katika Seneti kuhusu ugavi wa fedha kwa serikali za kaunti, wabunge nao sasa wamefufua wito kutaka waongezwe fedha za maendeleo.

Mvutano uliodumu kwa muda mrefu kuhusu mfumo utakaotumiwa kugawa fedha kwa kaunti ulifufua masuala mengi, ikiwemo kama pesa zinazotolewa hutumiwa vyema kwa manufaa ya wananchi.

Wakati ambapo idadi ya magavana wanaoandamwa na kesi za ufisadi inaongezeka, kuna wananchi wanaoamini viongozi wa kaunti hawakuwa na haki ya kudai kuongezwa fedha wala kulalamika kuwa wanapunguziwa.

Jumapili, wabunge kadha walifuchua mpango wa kupeleka hoja bungeni ili pesa za Hazina ya Kitaifa ya Ustawishaji Maeneobunge (NG-CDF) nazo ziongezwe kwa asilimia tano.

Sawa na magavana, wabunge wanadai kuwa wanahitaji pesa zaidi kuwahudumia wananchi. Hii si mara ya kwanza wabunge kutaka waongezwe pesa katika hazina hiyo, na pia kuna wakati walipopinga mipango ya kupunguziwa.

Kando na haya, kuna madiwani na viongozi wawakilishi wa wanawake bungeni ambao pia hupiganiwa kutengewa kitita kikubwa cha pesa kwa madai kuwa wanataka kupeleka maendeleo kwa wananchi.

Bila shaka, kuna viongozi wa kisiasa ambao wanafahamu fika kwamba hawatarudishwa mamlakani ikiwa wakazi wa maeneo yao hawataona maendeleo ya kuridhisha.

Hayo ni maeneo yaliyo na wapigakura wenye busara ambao huchagua viongozi kwa msingi wa uwezo wao kuleta mabadiliko bora kwa umma.

Kwa upande mwingine, kuna wale wanasiasa ambao wanajua wanachohitaji ni tikiti ya chama maarufu katika eneo lao ili washinde uchaguzini.

Kikundi hiki cha viongozi, pamoja na wale walioingia mamlakani kwa lengo moja la kujaza tumbo wakati mwingi huwa hawajali kutumikia umma. Kile wanachotaka ni kufuja mali ya umma na kujinufaisha kibinafsi pamoja na wandani wao.

Wito wowote wa kutaka fedha ziongezwe kwa hazina za kustawisha maendeleo unafaa uandamane na thibitisho kuwa wananchi hunufaika.

Bila hili, serikali kuu itaendelea kutiwa shinikizo kuongeza fedha mikononi mwa wanasiasa ilhali wananchi wanaoteseka kulipa ushuru watabaki kasika umaskini wao.

You can share this post!

Sonko aelekea korti ya rufaa kuhusu usimamizi wa jiji

Wabunge waapa kushinikiza NG-CDF iongezwe