TAHARIRI: Rais chukua hatua moja tu nchi ipone
Na MHARIRI
KUISHI Kenya sasa kunaudhi! Kunachosha! Kunatamausha! Hakukaliki! Kisa na maana, mnyonge sasa ananyongwa wala hana chake nchini humu.
Kinachoharibu hali yetu ni sakata baada ya sakata; tena si sakata ndogo bali wizi wa mabilioni. Sakata ya hivi majuzi zaidi kufichuliwa ni wizi wa makumi ya mabilioni.
Imebainika Kenya ilipoteza takribani Sh21 bilioni zilizotolewa na serikali kwa ajili ya ujenzi wa mabwawa ya maji ya Arror na Kimwarer katika Kaunti ya Elgeyo-Marakwet.
Ripoti za vyombo vya habari zinaonyesha kuwa washukiwa wa uhalifu huo walinunua ardhi ya Sh1 bilioni walipogundua kuwa ardhi hiyo ingenunuliwa kwa ujenzi wa mabwawa hayo kisha wakauzia serikali kwa Sh6 bilioni.
Aidha, mamilioni ya pesa yalitolewa kwa ununuzi wa taulo, mikate na maziwa pamoja na magodoro ambayo kwa hakika hayakuhitajika katika ujenzi wa mabwawa haya.
Je, Sh21 bilioni zina thamani gani? Pesa hizi zinaweza kuendesha kaunti mbili kuu nchini -Nairobi na Mombasa- kwa mwaka mmoja maadamu kaunti hizi hutengewa takribani Sh10 bilioni kila moja kwa mwaka.
Si ufisadi wa mabwawa tu, Kenya imeliwa katika kila kona. Si kashfa ya shirika la NYS, si ubadhirifu katika Wizara ya Afya, si katika shirika la Kenya Pipeline.
Haya yote ni matukio ya ufisadi yaliyoigharimu nchi hii mabilioni ya pesa ambayo, hakika yangeweza kutekeleza maendeleo makubwa zaidi nchini.
Sharti Rais Uhuru Kenyatta achukue hatua kali za kuangamiza zimwi hili la ufisadi, vinginevyo taifa hili liangamie katika muda mfupi ujao.
Inapozingatiwa kuwa Kenya ina madeni ya matrilioni ya pesa (takribani Sh5.3 trilioni), njia nzuri ya kulipa madeni hayo, na kwa wakati huo huo, iweze kufanikisha maendeleo, ni kuzima mianya ya kuiba pesa za mwananchi.
Hata kama ni utajiri, watu hawa wanaoiba wana utajiri wa kutisha huku mamilioni ya Wakenya wakihangaika na maisha.
Wengine hata wanakufa kutokana na njaa na umaskini ilhali wapo walioiba na kuficha mali ya nchi! Sharti jambo lifanyike haraka.
Maadamu Rais Uhuru ndiye mwenye mamlaka na usemi mkubwa kuhusu masuala muhimu yanayohusu nchi, achukue hatua madhubuti.