Makala

TAHARIRI: Ripoti ya maridhiano isiwagawanye raia

October 28th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na TAHARIRI

RIPOTI ya jopo la maridhiano (BBI) inatarajiwa kutolewa wakati wowote sasa, baada ya jopo hilo kukamilisha kazi yake wiki iliyopita.

Tangu tangazo lilipotoka kwamba Rais Uhuru Kenyatta tayari aliarifiwa ripoti imekamilika, kumekuwa na joto tele kuhusiana na ripoti hiyo ijapokuwa ilikuwa haijatolewa rasmi kufikia jana Jumapili.

Wale wanaoibua mdahalo zaidi ni viongozi wanaoegemea upande wa Naibu Rais William Ruto, ambao hawajaficha msimamo wao wa kupinga BBI kama itatoa pendekezo la kuongeza nyadhifa za utawala mkuu serikalini.

Wenzao wanaoshabikia upande wa Rais Kenyatta na Kiongozi wa ODM Raila Odinga wamesisitiza utekelezaji wa ripoti hiyo utakuwa muhimu kuleta usawa wa kijamii katika uongozi na ugavi wa rasilimali za taifa kwa njia ya haki.

Katika haya yote, mwananchi amebaki kuduwazwa na matamshi ya wanasiasa kwani hafahamu msema kweli ni nani ikizingatiwa ripoti inayobishaniwa haijulikani yaliyomo.

Ni matumaini yetu kuwa jopo la BBI halikutumia pesa, rasilimali na muda mwingi wa umma kufanikisha maslahi ya viongozi wa kisiasa kama inavyoshukiwa na baadhi ya wanaopinga shughuli zao.

Viongozi wa pande zote wajihadhari ili maridhiano yaliyokusudiwa yasiishie kuleta taharuki na mgawanyiko wa nchi.

Mdahalo wote unaoendelezwa uwe wa haki, unaoweka mbele matakwa ya mwananchi wa kawaida anayetamani maisha yake kuboreshwa na wala isiwe kwamba wanasiasa wanapiga domo tu kwa nia ya kulinda maslahi yao ya kibinafsi.

Wakati mwingi mwananchi wa kawaida hutegemea mwelekeo unaotolewa na wanasiasa kufanya maamuzi muhimu kuhusu utawala wa nchi.

Huenda mkondo huu ukarudiwa wakati ripoti itatolewa hasa endapo itapendekeza hitaji la kufanya marekebisho ya kikatiba.

Huu ni wakati mwingine mwafaka kwa raia kuwa macho, kusubiri kujionea yaliyomo katika ripoti ya BBI na kujifanyia uchanganuzi wa kina kisha hatimaye kujiamulia kama mapendekezo yaliyotolewa yanafaa au la.

Kuna uwezekano mkubwa pia kwamba huenda kukawa na masuala yatakayoachwa mikononi mwa wabunge kuamua jinsi yanastahili kutekelezwa.

Wito sasa ni kwa Ikulu kutenga muda hivi karibuni ili ripoti iwasilishwe kwa Rais ndipo itolewe wazi kwa umma.