TAHARIRI: Saratani: Hali yazidi kutisha
Na MHARIRI
HABARI za kuaga dunia Ijumaa kwa mbunge wa Kibra, Ken Okoth zilihuzunisha wengi na kuibua tena mjadala kuhusu ongezeko la visa vya saratani nchini.
Taifa limepoteza viongozi wawili wa haiba kubwa katika mwezi mmoja pekee; Bob Collymore na sasa Ken Okoth.
Wakenya wengine wengi pia wanaopoteza maisha yao kila siku kutokana na ugonjwa huu ambao kila uchao unazidi kutisha na kugadhabisha.
Kinachozuga akili zaidi ni kwamba si maradhi ambayo watu wanaweza kujua chanzo chake mapema ili kuepuka.
Sio kama ajali za barabarani ambazo, licha ya kuwa hazitabiriki, angalau umma unaweza kuambiwa kuhusu kutoendesha magari kwa kasi zaidi, au wakiwa walevi.
Sio kama malaria ambao tutaambiwa tulale ndani ya neti au tununue dawa za kuua mbu.
Sio kama virusi vya HIV/Ukimwi ambavyo tutaepuka mapenzi ya holela au kutumia kinga.
La, saratani ni maradhi ambayo hadi wa leo wanasayansi hawajaweza kueleza kwa bayana kinachoyasababisha.
Kile tunachojua ni kwamba inasababishwa na masuala ya urithi wa geni ndani ya mwili, masuala ya kimazingira, na mtindo wa maisha na hakuna ufafanuzi wa kihakika kuhusu mtindo upi haswa kwa sababu kama ni sigara, kunao wanajikuta kupata saratani na wanaoponyoka.
Ki msingi, haijajulikana ni nini ambacho binadamu anafaa kufanya kuepuka maradhi haya na hapa ndipo wasiwasi unaongezeka kwa sababu kadri siku zinavyosonga ndivyo maradhi haya yanavyopiga kumbo maradhi yaliyojulikana kwa muda mrefu kuwa yanayoua watu wengi nchini.
Takwimu zilizochapishwa kwenye gazeti la Daily Nation Alhamisi zilionyesha kwamba visa 47,887 vya saratani huripotiwa nchini kila mwaka huku ugonjwa huo ukishikilia nambari tatu katika orodha ya chanzo cha vifo nchini.
La kusikitisha zaidi, nyingi ya visa hivyo huishia katika maisha kupotea. Saratani ya koo pekee, kati ya visa 4,380 vilivyoripotiwa, 4,351 walipoteza maisha kwa maana kwamba ni watu 31 pekee waliofaulu kupambana na kupona.
Haifai kuendelea na maisha kama kwamba jinamizi hili ni upepo upitao.
Ukweli ni kwamba kuna vigezo ambavyo havikuwepo awali, ambavyo vinachangia katika ongezeko la ndwele hii. Sharti wadau katika Afya wabuni mikakati ya utafiti kutambua haswa kinachoendelea huku juhudi kabambe zikiwekwa kuhusu matibabu na matunzo kwa wagonjwa wa saratani.