Makala

TAHARIRI: Serikali iimarishe vifaa vya shule

October 16th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MHARIRI

NI aibu iliyoje kusoma taarifa za shule ya msingi ya umma yenye zaidi ya wanafunzi 400 ilhali haina choo hata kimoja cha kujisaidia.

Amini usiamini, watoto hao 450 na walimu wao sita huenda haja kichakani!

Isitoshe, kuna madarasa mawili pekee katika shule nzima ilhali masomo yanaanzia darasa la chekechea hadi la sita.

Madarasa hayo yalijengwa kwa ufadhili wa Hazina ya Ustawi wa Maeneobunge (CDF) na utawala uliopita.

Wanafunzi wanaoelekea darasa la saba hulazimika kuhamia shule nyinginezo ili kukamilisha masomo yao.

Masomo hapa ni kwa zamu: chekechea wanaingia asubuhi na kuondoka alasiri ili darasa la tatu waingie kutumia chumba chao.Darasa la kwanza na pili wanabadilishana alasiri na darasa la nne hadi sita, ili watumie chumba hicho kinachogawanywa sehemu tofauti.

Ndivyo hali ilivyo katika shule ya msingi ya Mwigalenii katika Wadi ya Mwanamwinga, Kaunti ya Kilifi. Hii ni licha ya kuwa shule hiyo ya eneobunge la Kaloleni imekuwepo tangu 2006 iliposajiliwa na serikali.

Ni masimulizi ya kutamausha. Huu ni utepetevu wa kusikitisha. Serikali, wizara, viongozi wa hapo na wadau katika sekta nzima ya elimu wanastahili lawama.

Kwanza, afya ya wanafunzi iko hatarini. Wanakodolea macho mkurupuko wa maradhi ya kuambukizwa kupitia maji-taka kama vile kipindupindu. Pili, usalama wao uko hatarini. Kuna hatari ya kukumbana na wanyama hatari kama vile nyoka.

Tatu, kuna hatari kubwa ya wanafunzi wakorofi kutumia fursa hiyo kuwavizia na kuwadhulumu wenzao, kimapenzi na vinginevyo.

Inasemekana takriban shule 18 za Kaloleni ni mbovu. Je, mbunge wa hapo anajua hali hiyo inayokumba wanafunzi katika eneo lake?

Wizara ya Elimu imekuwa ikipokea mgao mkubwa wa bajeti za kitaifa.

Mwaka huu 2019/20 takriban Sh1.5 bilioni zilitengwa kwa ujenzi na uimarishaji wa miundo-msingi kama vile madarasa.

Mbona Wizara ya Elimu isitumie kiasi cha pesa hizo kuimarisha shule ya Mwigalenii? Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) haijapeleka walimu shuleni humo, hivyo walimu na wazazi ndio hujitafutia walimu.

Je, Sh3.2 bilioni za kuajiri walimu zimetumika vipi iwapo shule kama hii haikupewa umuhimu? Tusisubiri maafa ili kuokoa shule hii na nyinginezo zilizo katika hali mbovu nchini.