TAHARIRI: Serikali ikaze kamba kwa homa ya China
Na MHARIRI
SERIKALI ya Kenya ni sharti ijitokeze kwa ukakamavu zaidi kuondolea wananchi hofu kuhusu virusi vya Corona ambavyo vinazidi kuenea kwa mataifa mbalimbali ulimwenguni.
Humu nchini, kuna mtu mmoja aliyelazwa hospitalini Jumanne akiwa na dalili za ugonjwa huo ulioibukia China mwishoni mwa mwaka uliopita.
Jambo la kwanza ambalo serikali inastahili kufanya ni kuimarisha jinsi inavyotoa habari kwa wananchi.
Kufikia sasa, habari za serikali zinazofikia umma kuhusu ugonjwa huo ni kupitia taarifa kwa vyombo vya habari.
Ijapokuwa Wizara ya Afya imekuwa ikitoa taarifa kwa wanahabari kuhusu hatua zinazoendelezwa kuzuia uwezekano wa maambukizi ya ugonjwa huo hatari kuingia nchini, hatujaona ikielimisha umma ipasavyo.
Inavyoonekana, jukumu hilo limeachiwa vyombo vya habari pekee ambavyo, tofauti na serikali, havina uwezo wa kufikia kila pembe ya nchi na zinaweza tu kusambaza habari hizi kadri na uwezo wao.
Bila serikali kuelimisha umma moja kwa moja, kuna hatari ya wananchi kuishi kwa hofu wakishuku mtu yeyote atakayeonekana mdhaifu kiafya.
Kando na haya, hatua ambazo serikali inachukua kuhusu ugonjwa huo zinafaa zidhihirishe imejitolea kikamilifu kulinda raia wake.
Kwa mfano, jana, raia wengi walishtuka waliposikia shirika la ndege la kitaifa la Kenya Airways litaendeleza safari zake za kuelekea China kama kawaida.
Hii ilitokea wakati ambapo mataifa mengine mengi hasa ya magharibi yanasitisha safari zao China au kuzipunguza.
Jambo jingine lililoshtua ni hatua ambazo serikali ilichukua kwa wasafiri waliokuwa wamekuja Kenya kwa ndege moja na mwanafunzi aliyeshukiwa kuambukizwa ugonjwa huo.
Jumatano ndipo ilifahamika kuna uwezekano baadhi yao huenda walikaribiana na mgonjwa huyo na hivyo ikalazimu serikali kutafuta wasafiri wote ili hali yao ya afya ifuatiliwe kwa karibu kwa wiki tatu.
Hii inaonyesha kulikuwa na utepetevu kwa kiasi fulani kwani wasafiri wote wangeruhusiwa tu kwenda nyumbani moja kwa moja kama hapakuwa na yeyote kati yao aliyekuwa na dalili za kuugua.
Serikali ina jukumu kubwa kulinda maisha ya raia wake. Wakati kama huu, masilahi ya kibiashara na diplomasia hayafai kupewa uzito kuliko hitaji la kulinda binadamu.