TAHARIRI: Serikali isilemaze Wakenya kwa kodi
Na MHARIRI
WANAOENDESHA biashara mitandaoni sasa wanatarajia kutozwa ushuru wa asilimia 1.5 ya mapato yao ya jumla kutokana na biashara wanazoendesha.
Serikali imetangaza harakati hizo katika juhudi za kuhakikisha kuwa inajazia mapengo yake ya ushuru.
Akiwasilisha bajeti ya mwaka wa fedha wa 2020/2021, Waziri Ukur Yatani alitangaza kuwa serikali inalenga kuweka utaratibu wa kutoza ushuru biashara zinazoendeshwa kidijitali
Katika siku za hivi punde biashara za kidijitaji zimeonekana kunawiri huku wengi wakihisi kuwa ni nafuu kuliko kukodisha maduka ambapo gharama ya kuyamudu huwa juu.
Biashara nyingi zimeweka soko zake mitandaoni na katika kipindi cha miezi mitatu baada ya kuzuka kwa maradhi yanayotokana na virusi vya corona, Wakenya wengi wamehamia kuendesha biashara zao mitandaoni.
Idadi hii imeongezeka huku wengi wakitafuta njia za kuwasaidia kupata mapato baada ya kupoteza ajira ama kulazimika kuchukua likizo ya lazima bila malipo.
Pia inafaa kubainika kuwa wengi waliolekea kuendesha biashara zao mitandaoni ni vijana ambao serikali imeendelea kuwaahidi kuwa itawabunia nafasi za ajira. Lakini kwa sasa kufuatia maambukuzi ya maradhi ya corona, huenda ikawa vigumu kutegemea serikali kubuni nafasi hizo za kazi.
Tunatambua kuwa serikali inahitaji kupata ushuru kuweza kuendesha nchi na kuhakikisha kuwa masuala na mahitaji muhimu katika sekta mbalimbali yanaendelezwa kupitia ushuru huu. Lakini inapoendelea kuangalia harakati hizi, inafaa pia kuzingatia suala la vijana na jinsi ya kuwainua kwa kuhakikisha kuwa wana mazingira yanayofaa kuendeshea biashara zao.
Bajeti hiyo ya Sh2.79 trilioni ina upungufu wa Sh840.6 bilioni kumaanisha kuwa lazima serikali iangalie mikakati zaidi ya kuongeza mapato yake ya ushuru. Lakini inapolenga kufanya hivyo, pia ikumbuke pigo ambalo limeathiri Wakenya kwa sasa hasa kutokana na janga la corona na kuzuia kuwaongezea mzigo zaidi inapotathimini ushuru kwa bidhaa mbali mbali hasa zile muhimu na za msingi.
Bajeti hiyo hata hivyo pia inaangazia mpango wa kazi mitaani ambao bila shaka unalenga vijana. Hili ni jambo zuri ingawa pia utaratibu wa jinsi vijana hawa wanavyosajiliwa kwa mpango huu unafaa kuwa na uwazi na pesa hizo zisiporwe na walaghai.