Makala

TAHARIRI: Serikali iwape moyo wakulima

October 9th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MHARIRI

MSIMU wa mavuno umeshaanza katika maeneo mbalimbali ya Bonde la Ufa.

Baadhi ya wakulima wameanza kuvuna mahindi yao huku wengine wengi wakitarajiwa kufanya hivyo katika wiki chache zijazo.

Mavuno hayo yataleta afueni kuu kwa mwananchi wa kawaida, ambaye amelazimika kununua pakiti ya kilo mbili za unga wa mahindi kwa zaidi ya Sh120 kutoka Sh85 mwezi Januari, kufuatia uhaba wa nafaka hiyo muhimu nchini.

Ugali ndio lishe kuu ya Wakenya na inasikitisha kwamba miaka 56 baada ya uhuru, serikali imeshindwa kuzalisha mahindi ya kutosheleza wananchi wake.

Hii ni licha ya kwamba wakulima nchini huwa na mahindi katika ghala zao, ila serikali hukataa kununua zao lao kwa bei nzuri.

Kwa mfano, wakati wa mavuno ya mwaka jana wakulima walitaka bei wastani ya Sh3,200 kwa kila gunia la kilo 90 la mahindi yao, lakini serikali ilishikilia kwamba itanunua tu kwa Sh2,300.

Kinaya ni kwamba, serikali huwa radhi kununua kwa bei ya juu mahindi yanayoagizwa kutoka nje kunapozuka upungufu mkubwa katika viwanda vya usagaji.

Upungufu huo ulishuhudiwa Aprili na viwanda kadha katika maeneo ya North Rift na Magharibi vikafungwa.

Serikali ililazimika kuruhusu mahindi kutoka mataifa ya kanda kuokoa jahazi. Wasagaji waliishia kununua gunia moja kwa kati ya Sh3,300 na Sh3,400.

Ni wazi kwamba sekta ya mahindi imetekwa na makundi ya wafanyabiashara mabwanyenye wanaojinufaisha kutokana na uhaba wa mara kwa mara, huku mkulima mdogo pamoja na mwananchi wa kawaida akiumia.

Msimu huu wa mavuno ukiendelea kushika kasi, tunatazamia kuwa viwanda vya kusaga mahindi vitapunguza bei ya unga.

Pili, tunatumai serikali imeweka mikakati kununua mahindi yote ya wakulima ili kuzuia uhaba mwaka 2020.

Kuambatana na hilo, tunatarajia serikali kununua mahindi hayo ya wakulima kwa bei bora.

Walitumia hela nyingi kununua pembejeo msimu huu hasa ikikumbukwa kwamba serikali ilikosa kuwasilisha kwao mboleo na pembejezo zinginezo zilizopunguzwa bei. Hivyo, wakulima watapata hasara kubwa endapo mahindi yao yatanunuliwa kwa chini ya Sh3,500.