• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 3:55 PM
TAHARIRI: Shirika la Posta lahitaji uvumbuzi

TAHARIRI: Shirika la Posta lahitaji uvumbuzi

Na MHARIRI

KESHO Jumatano Kenya inaungana na ulimwengu kuadhimisha miaka 145 ya Siku ya Posta Duniani.

Sherehe hiyo itakayoongozwa na Waziri wa Habari, Teknolojia na Mawasiliano, Bw Joe Mucheru, itaangazia nguzo tatu kuu: Uvumbuzi, Ujumuishaji na Ushirikishaji.

Ni vizuri kwamba serikali kupitia Shirika la Posta nchini inatambua uvumbuzi kuwa mojawapo ya nguzo kuu za ustawi.

Kwa miaka kadhaa sasa, shirika la Posta limekuwa likifunga afisi zake katika maeneo mengi nchini. Hata yale majengo yaliyopo kwa sasa yamegeuzwa kuwa vituo vya utoaji huduma mbalimbali za serikali, maarufu kama Huduma Centre.

Masanduku ya Posta yamesalia kuwa ya kutumiwa mizigo na barua chache, hasa za mashirika ya serikali na kampuni kubwa.

Takwimu za Halmashauri ya Mawasiliano nchini (CA) zinaonyesha kuwa barua zinazotumwa nchini zilipungua hadi milioni 47, ambacho ni kiwango cha chini zaidi katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.

Mwaka wa 2010 barua milioni 109 milioni zilitumwa kupitia shirika la Postal Corporation of Kenya.

Kuwepo kwa huduma za mitandao kwa urahisi katika sehemu nyingi za nchi kumefanya Wakenya wengi kuwasiliana kwa njia ya baruapepe, ujumbe mfupi kwenye simu, na sasa hivi kuna mitandao ya kijamii kama vile Facebook na WhatsApp.

Kinyume na miaka 10 iliyopita ambapo Shirika la Posta lilitegemewa kupeleka mizigo kutoka eneo moja hadi jingine, sasa hivi kuna zaidi ya kampuni 1,000 za kibinafsi zinazotekeleza jukumu hilo, zikiongozwa na zile za mabasi.

Kuwekwa soko huru la kusambaza mizigo kunafanya Wakenya wawe na uhuru wa kuchagua kampuni ya mizigo ya kutumia. Shirika la Posta likiwa la serikali, linapaswa kuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kusafirisha mizigo hiyo.

Kinacholikosesha biashara ni wafanyakazi wenye uzembe, wanaoamini kuwa kwa vile wameajiriwa na serikali, hata wakiwa wajeuri au wasipohudumia wateja kwa njia ya haraka na salama, mishahara yao itaingia tu mwisho wa mwezi.

Tunapojiandaa kuadhimisha Siku ya Posta Duniani, serikali yapaswa kuchukua hatua za kufufua shirika la Posta, na kuzuka na mbinu za kisasa za kuvutia wateja ambao wanazidi kuongezeka.

Ingawa kuna ushindani mkubwa wa kibiashara, kupitia uvumbuzi, shirika la Posta inaweza kurejelea umaarufu katika utoaji huduma za mawasiliano.

You can share this post!

Matiang’i awataka viongozi wa kidini kuisaidia...

NGILA: Ukosefu wa ufadhili unavuruga ukuaji wa teknolojia

adminleo