TAHARIRI: Siasa: Raia wazingatie sera si maneno matupu
Na MHARIRI
KAMPENI zikiwa zimeanza kwa uchaguzi mdogo katika eneobunge la Msambweni na chaguzi nyingine ndogo, ni muhimu kwa viongozi kuendesha siasa ambazo zitauza sera na si kugawanya Wakenya.
Katika siku za hivi punde, nchi imeshuhuhudia joto la kisiasa likipanda kuhusiana na masuala mbalimbali yanayoendelea nchini. Hali hiyo, imeelekeza serikali kuweka kanuni zinazodhamiria
kushusha joto hilo, hasa baada ya vijana wawili kuuawa kwenye vurugu Kaunti ya Murang’a, Naibu Rais, William Ruto alipokuwa ziarani.
Ni muhimu kwa wanasiasa kutambua kuwa ni rahisi kuangamiza nchi kwa maneno ya vinywa vyao. Baadhi yao wana wafuasi tele na ambao hawatasita kufuata yale wanayowaeleza. Lakini baada ya taifa kushuhudia umwagikaji wa damu baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2007, kushuhudia ama kusoma yaliyojiri katika mataifa kama Rwanda, basi wananchi hawana budi kuwa makini kuhakikisha kuwa wanadumisha uwiiano na utangamano nchini.
Wananchi wanafaa pia kufikiria kuhusu maisha yao binafsi badala ya kuamua kufuata upepo ama kuzingatia matamshi ya wanasiasa. Katika kipindi hiki, Uchumi wa Kenya sawa na mataifa mengi duniani, umepata pigo kuu kutokana na janga la corona. Idadi kubwa ya watu wamepoteza ajira, na kukosa njia za kujikimu. Wengi pia wanajaribu kufanya hili na lile, waweze kumudu mahitaji yao na ya familia zao. Kwa hivyo, itakuwa makosa ikiwa raia watasahau hali ngumu ambayo wamepitia kutokana na makali ya athari za corona na kufuata wanachosema wanasiasa bila kuzingatia maslahi yao wenyewe.
Ni muhimu pia kwa raia kutambua kuwa mchango wao, fikra zao zinastahili kuwaongoza katika maamuzi yao hasa kuhusiana na viongozi. Mara nyingi wakati wa uchaguzi, watu huandama chama au mwanasiasa kwa sababu ya kabila lakini baadaye wenyewe wakaishia kulalama kuwa hawajasaidika.
Lazima wananchi wenyewe wabadilishe jinsi wanavyofanya maamuzi kuhusiana na watu wanaotaka kuwaongoza. Hii itasaidia wanasiasa kuelekeza siasa zao kwa sera na malengo yao badala ya kueneza chuki na uhasama au kugawanya raia.
Raia wana uwezo wa kuamua mwelekeo wa nchi hasa kuhakikisha kuwa ahadi zinazotolewa zinatimizwa, kukomesha ufisadi na kudai maendeleo. Hadi fikra zitakapotua hapo na wengi kufunguka macho kuwa uwezo upo kwao, wanasiasa wataendelea kutawala akili na fikra zetu na kutuweka “mateka wao.’