• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 7:12 PM
TAHARIRI: Soka ya Kenya iache utegemezi

TAHARIRI: Soka ya Kenya iache utegemezi

Na MHARIRI

TANGU msimu mpya wa Ligi Kuu nchini (KPL) uanze, zipo dalili hatari ambazo zimeonekana. Changamoto kuu mwaka huu ni kwamba lipo tatizo la ufadhili.

Mwanzo, zipo timu ambazo kabisa kabisa zimeshindwa kukidhi mahitaji ya kimshahara kwa wafanyakazi na wachezaji wao. hali hii imewafanya baadhi ya wachezaji kutofika kwa mazoezi kama ilivyo ada kabla ya michuano. Bila shaka hali kama hii inapotokea, timu hizi zitashuhudia matokeo duni uwanjani.

Pili, tatizo halikuishia kwa timu pekee; kampuni iliyo na jukumu la kuendesha ligi kuu nchini yaani KPL haijasazwa. KPL imeshindwa kulipa ada za waamuzi katika baadhi ya mechi na hivyo kuziachia timu zinazochuana mzigo wa kulipa ada hii. Hii ni hali ya kusikitisha mno.

Matatizo haya mawili yanatishia kulemaza soka nchini Kenya. kabla ya hizi changamoto, soka ya Kenya ilikuwa imeshuhudia uthabiti kwa kipindi kirefu. Uthabiti huu ulitokana na kuwepo kwa wadhamini.

Kwanza, Kampuni ya Supersport ilikuwa imeingia ubia na KPL ambapo ilikuwa inatoa ufadhili kisha nayo inapeperusha mechi za ligi kuu katika runinga. Hii ilikuwa hatua kubwa sana iliyopiga jeki soka ya Kenya.

Hata hivyo, baada ya KPL kuongeza idadi ya timu zinazocheza katika KPL kutoka 16 hadi 18 kinyume na mkataba, Supersport iliondoa ufadhili wake na pia kukoma kupeperusha mechi zetu katika chaneli zake. huo ndio ulikuwa mwanzo wa masaibu.

Baadaye, kampuni za kamari zilipopata leseni ya kufanya kazi nchini baadhi yazo na kwa kweli zile kuu zilijitoa mhanga kutoa ufadhili kwa timu kuu nchini.

SportPesa walitoa ufadhili kwa timu za Gor Mahia na AFC Leopards.

Kampuni ya Betin kwa upande wake ilijitokeza kufadhili shughuli za timu ya taifa Harambee Stars. Kampuni hizi mbili zilikuwa mdau mkubwa sana wa spoti kwa ujumla nchini Kenya.

Hata hivyo, baada ya mapambano ya serikali na kampuni hizi kuzuka, mambo yamebadilika mno.

Mswahili husema ‘mwenye nguvu mpishe.’

Serikali iliweka sheria kali za mchezo wa kamari nchini na kampuni zikafunga biashara zao nchini na kutosa timu zilizozitegemea katika lindi la masaibu ya udhamini.

Umefika wakati kwa soka ya Kenya kuukubali uhalisia huu na badala yake kuanza kuwekeza ili kuepuka utegemezi.

Ni kwa njia hii pekee ndipo klabu za soka nchini na KPL itapata uthabiti na hivyo kuepuka kuyumbishwa na masilahi, hali au matamanio ya wadhamini.

You can share this post!

Patashika yazuka katika mazishi ya mzee

MWANAMKE MWELEDI: Sanaa inafanya avume ugenini

adminleo