• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 7:55 PM
TAHARIRI: Spoti ya kina dada ipewe umuhimu

TAHARIRI: Spoti ya kina dada ipewe umuhimu

Na MHARIRI

ISHARA zimeanza kuonyesha kwamba michezo ya wanawake inaweza kuiletea nchi hii manufaa makubwa kuliko ilivyodhaniwa katika miaka ya awali.

Hii imedhihirika wazi hasa kupitia kwa kandanda ya wanawake ambapo vikosi vya taifa vya soka na voliboli kupitia kwa timu za Harambee Starlets na Malkia Strikers.

Mbali na kuzolea Kenya sifa kwa kutawala voliboli ya Afrika na hata kujaribu katika medani ya ulimwengu, Malkia Strikers imewawezesha wasichana wengi kupata ajira katika klabu za kigeni.

Mercy Moim ambaye amewahi kucheza voliboli ya kulipwa Finland, Thailand na Azerbaijani na Jane Wacu ambaye amewahi kucheza Ufaransa na Ushelisheli ni mifano bora wa wanavoliboli ambao wamevuna pato zuri kutokana na talanta zao.

Wanasoka wa Harambee Starlets wanaovuna jasho lao kwa kucheza klabu maarufu ulimwenguni ni Vivian Corazone Aquino aliye Ureno kwa sasa, Annedy Kundu na Ruth Ingosi walio Cyprus na Esse Akida anayecheza nchini Uturuki.

Mafanikio haya yana maana kuwa iwapo serikali itatilia maanani zaidi michezo ya wasichana, kuna uwezekano mkubwa kuwa, chipukizi wengi wa kike wenye vipawa watapata fursa ya kujizumbulia riziki na hivyo basi kuzifaa familia zao pamoja na taifa kwa jumla.

Pale ambapo timu za wanaume zimeshindwa kufanya hivyo, baadhi ya timu za wanawake zimekuwa zikifana. Hivyo basi ni muhimu kutilia mkazo fani ambazo wanawake wanafanya vyema hasa katika medani za kimataifa.

Hii haimaanishi, hata hivyo, kuwa timu za wanaume zisisaidiwe kujiinua, ila ni bora kuwa juhudi zinapoendelea kufanywa ili nazo ziinuke, za wanawake zinazotia fora zipewe kila udhamini na usaidizi wa kutosha ili zitawale zaidi.

Iwapo jitihada zitawekwa zaidi katika makuzi ya mchezo wa kandanda ya kinadada, kwa mfano, hivi karibuni tutashuhudia wanasoka wengi wa jinsia hiyo wakisajiliwa na klabu maarufu za kigeni ambazo bila shaka zitawalipa vizuri na hivyo basi kusaidia taifa hili kujiendeleza kichumi.

Sekta ya michezo katika siku zijazo imeonyesha dalili za kukua kwa kasi na hivyo basi mataifa yatakayojiandaa kuchukua nafasi hizo ndiyo yatakayonufaika. Nasi Kenya tusiachwe nyuma pale wanda la spoti litakapochipuza matunda zaidi.

You can share this post!

Hofu ya Corona yatikisa Kenya

MUTUA: Serikali iache masihara kuhusu virusi vya Corona

adminleo