TAHARIRI: Stars waliponzwa na benchi la ufundi
Na MHARIRI
TIMU ya taifa ya Harambee Stars ilirejea nyumbani kimyakimya mnamo Alhamisi baada ya kubanduliwa kwa aibu kwenye fainali za Kombe la Afrika zinazoendelea nchini Misri.
Ilikuwa mojawapo ya timu zilizotoka jijini Cairo na kapu zito la magoli baada ya kufungwa jumla ya mabao saba.
Kocha Sebastien Migne na kikosi chake cha wataalamu kilionekana kukosa maarifa kila mara Harambee Stars ilipokutana na timu kubwa barani; Algeria na Senegal.
Hasa katika mechi ya Senegal ilikuwa dhahiri kuwa Harambee ingeshindwa mechi hiyo licha ya kukwepa kufungwa katika kipindi cha kwanza. Sababu kuu ya kulazwa kwa Kenya ni mbinu aliyotumia kocha huyo; kutumia mchezo wa ulinzi.
Imefahamika kwingi katika ulimwengu wa soka kuwa mbinu ya kuzuia aghalabu huwa haifaulu.
Hii ni kwa sababu timu pinzani hupewa fursa ya ‘kukita kambi’ katika ngome yako hivyo basi huweza kupata nafasi nyingi za kufunga ikiwemo kupata penalti kutokana na makosa ya mabeki.
Falsafa kubalifu huwa ni, mbinu nzuri ya kujikinga katika soka ni kushambulia. Unaposhambulia timu pinzani hubabaika kujizuia mbali na kukupa nafasi ya kunufaika kutokana na makosa ya ulinzi wao.
Katika mchezo huo wa Senegal, ilikuwa vigumu kwa mchezaji mmoja; mshambuliaji Michael Olunga kupata mpira ili ashambulie maadamu ilikuwa vigumu kuutoa mpira kwenye himaya yao.
Olunga abanwa
Hata baada ya kuipata mipira kwa nadra, Olunga hangeenda nayo mahali maadamu kila mara alibanwa sana na walinzi wa Senegal.
Laiti Migne na kikosi chake wangejifunza kutokana na timu ndogo zilizokuwa zimefana kwa kutumia mchezo wa kushambulia! Bukini yaani Madagascar, kwa mfano, walikuwa wameduwaza Nigeria siku moja kabla ya mechi hiyo ya Kenya, kwa kuwarapua majabali hao wa bara mabao 2-0.
Kesho yake Benin ikicheza na Cameroon, iliwabana miamba hao hadi ikafaulu kutoka sare. Siku chache kabla ya mechi ya Stars, Uganda ilikuwa imeitatiza vibaya Misri, japo ilishindwa hatimaye.
Hivyo basi, swali linaloibuka ni je, kwa nini Kenya iliogopa jinsi hiyo ilhali siku hizi hata timu ndogo haziogopi zile kubwa?
Mbali na mbinu hafifu za Kenya, kocha Migne alikuwa ameanza kukosea kwa kuwaepuka wanasoka mahiri kama vile Allan Wanga na Jesse Were katika kikosi chake pamoja na kupanga vikosi vilivyocheza mechi hizo za AFCON kwa namna isiyopendeza.
Sharti dosari hizi zitambuliwe na kurekebishwa upesi iwapo tuna nia ya kupiga hatua ya maana siku zijazo.