Makala

TAHARIRI: Suluhu ya Kenya si madeni zaidi

October 11th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MHARIRI

MNAMO Jumatano, wabunge waliipa serikali idhini ya kukopa madeni yanayofika jumla ya Sh9 trilioni.

Awali Kenya imekuwa ikiruhusiwa kuchukua jumla ya Sh6 trilioni pekee.

Hatua hii ni hatari sana kwa taifa hili ambalo kwa sasa linaendelea kupitia changamoto kubwa za kiuchumi. Kutokana na ukosefu wa pesa pamoja na kazi, Wakenya wengi kwa sasa wamepoteza uwezo wao wa kununua bidhaa na huduma. Wengi wanaishi maisha ya kijungu jikoni tu huku wakisitisha shughuli zozote za maendeleo.

Serikali kwa upande mwingine inatatizika sana kutimiza majukumu yake ya kimsingi kama vile kuzisambazia kaunti mgao wazo kwa muda unaofaa mbali na kuonekana kutatizika kulipa mishahara.

Suluhu kubwa ya Kenya kwa sasa ingekuwa kusitisha miradi yote ya maendeleo, hasa miradi mipya ambayo aghalabu ndiyo hulazimu nchi kukopa kila mara. Kadhalika, tatizo sugu la ufisadi limekuwa likichangia katika kuzorota kwa uchumi wetu.

Kenya inahitaji muda wa kutokopa kama suluhu ya kimsingi kwa tatizo hili. Kwa sasa deni la Kenya linaelekea Sh6 trilioni, hii ikiwa takribani asilimia 60 ya thamani ya mali ya Kenya (GDP).

Kwa kusogeza deni hilo hadi Sh9 trilioni, hiyo ina maana kuwa sasa taifa hili linaweza kukopa madeni yanayotoshana na utajiri wake; asilimia 100. Hatua hii kadhalika ina maana kuwa, iwapo Kenya itashindwa kulipa deni hilo, wadeni wake wanaweza kuamua kuiuza nchi hii pamoja na raia wake ili wapate pesa zao.

Serikali yafaa ijifunze kutokana na Ugiriki ambayo ilitatizika sana na mtikisiko wa kiuchumi ulioanza mwaka wa 2009. Ugiriki ilikuwa na madeni ya zaidi ya asilimia 100 ya utajiri wake.

Iwapo miradi inayolazimisha Kenya kuchukua madeni zaidi itasimamishwa, hiyo inamaanaisha katika kipindi cha miaka mitatu, kwa mfano, Kenya itapunguza deni lake kwa takriban Sh2.5 trilioni; yaani kwa sasa Kenya hulipa Sh800 bilioni kwa mwaka kama madeni.

Hii, aidha inamaanisha kuwa, deni la Kenya litakuwa limeshuka kutoka karibu Sh5.8 trilioni hadi Sh3.3 trilioni huku GDP yake ikiwa imeongezeka kwa karibu jumla ya Sh11 trilioni, kwa kuzingatia ukuaji wa uchumi wa asilimia sita kwa mwaka.

Iwapo deni hilo litashuka kiasi hicho huku uchumi ukiendelea kukua, taifa hili litaanza kujisimamia kimaendeleo badala ya kutegemea madeni.