TAHARIRI: Taifa lipewe sababu za kujivunia Katiba
Na MHARIRI
TANGU 2010 Agosti umekuwa mwezi muhimu kwa Wakenya kwani huwakumbusha kuhusu hatua za mwisho zilizowezesha nchi kupata katiba iliyosifika kuwa ya mageuzi makubwa.
Mwaka huu, maadhimisho hayo yatakuwa yanagonga miaka 10.
Wakenya walikuwa na wingu la matumaini kwamba maisha yao yangebadilika kabisa wakati walipofurika kupigia kura Katiba mpya 2010. Waliamini viongozi wangetekeleza yote yaliyomo kwa manufaa ya umma.
Japo baadhi ya masuala yameafikiwa na kutekelezwa, mengine muhimu yamepuuzwa na serikali. Utawala wa mfumo wa ugatuzi ambao ulikuwa mojawapo ya masuala makuu katika Katiba, umekosa kuafikia malengo yake yaliyokusudiwa.
Mivutano kati ya serikali kuu na za kaunti kuhusu ugavi wa fedha na majukumu ya kikatiba, hutatiza huduma kwa mwananchi.
Vilevile, uporaji wa pesa za umma katika serikali za kaunti umechangia kaunti nyingi kutopiga hatua kimaendeleo.
Katiba pia ilipendekeza theluthi mbili za nafasi za uongozi kwenye sekta na tume mbalimbali ziwaendee wanawake nchini.
Hata hivyo, mswada wa Jinsia ulikosa kupitishwa bungeni kwa mara ya nne mnamo Februari, 2019 hata baada ya kupigiwa upatu na Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga.
Pia ubabe na tofauti za kisiasa kati ya asasi za bunge, mahakama na afisi ya Rais mara nyingi zimepiga breki utekelezaji kikamilifu wa yaliyomo kwenye Katiba.
Licha ya Katiba kutoa uhuru katika asasi hizo, kumeshuhudiwa hali ambapo Afisi ya Rais inalaumiwa kwa kujaribu kuvuruga haki hiyo ya kikatiba.
Kwa ufupi, taifa bado lina kibarua kigumu kutekeleza kikamilifu Katiba ya 2010 kwa sababu kuna masuala kadhaa ya uongozi, haki za raia, umoja wa taifa, ugavi wa mapato na mamlaka pamoja na ugatuzi kati ya mengine kupuuzwa.
Haya ni masuala ambayo yalifaa kutatuliwa kabla hata ya kuanza kuzungumzia marekebisho ya Katiba yanayopigiwa debe chini ya Mpango wa Maridhiano (BBI).
Hatuwezi kutarajia mabadiliko chini ya Katiba yoyote ile ikiwa hatuna heshima kwa yaliyomo katika Katiba ya sasa, iliyosifiwa kimataifa kama ya kupigiwa mfano.