TAHARIRI: Takwimu zitumiwe kukomesha ajali
KITENGO CHA UHARIRI
RIPOTI iliyotolewa majuzi na Mamlaka ya Usalama Barabarani (NTSA) ilionyesha kuwa idadi kubwa ya ajali hutokea wikendi, na huhusisha vijana.
Ajali hizo zinazohusisha vijana wa umri wa kati ya miaka 29 hadi 39 zinafaa kuchukuliwa kwa uzito. Kuna uwezekano mkubwa kwamba hizi ni ajali ambazo hutokea kwa ajili ya uendeshaji magari kiholela hasa wakati watu wakiwa walevi.
Hii ni kutokana na kuwa, wikendi ndipo vijana wengi huenda kujivinjari katika sehemu mbalimbali mijini na hata vijijini.
Suala kuhusu ajali barabarani limekuwa donda sugu katika nchi hii kwa miaka mingi. Takwimu kama hizo za NTSA hazifai kuhifadhiwa tu baada ya kutangazwa, bali zinafaa kutumiwa kuongoza uundaji wa sera na sheria ambazo zitasaidia kupunguza ajali barabarani.
Kwa kuzingatia matukio ya ajali, umri wa wahusika, maeneo ambapo ajali hutokea na muda wa ajali hizo, wachanganuzi na wataalamu wanaweza kufahamu tatizo liko wapi na hatimaye kupendekeza hatua zinazofaa kuchukuliwa na asasi husika.
Tunaishi katika enzi ambapo maamuzi yoyote yanayofanywa yanafaa yazingatie kila jambo lililopo na hilo haliwezekani bila uchunguzi na utathmini wa kina. Teknolojia za kisasa pamoja na maarifa mengi tunayojivunia nchini humu yanatosha kutusaidia kupata suluhisho la kudumu, sio tu kuhusu ajali za barabarani bali pia changamoto nyinginezo zinazotukumba kitaifa.
Mashirika tofauti ya serikali hutumia rasilimali tele za nchi kufanya uchunguzi na kukusanya data kuhusu matukio mbalimbali.
Kinachosikitisha ni kuwa, takwimu hizo wakati mwingine husahaulika punde baada ya kutangazwa kwa umma, badala ya kutumiwa kutoa mwongozo kuhusu jinsi ya kurekebisha hali kwa njia itakayofaidi wananchi.
Kila mwaka, maelfu ya watu hufariki ajalini huku wengine wengi wakibaki na majeraha ya kudumu. Matukio haya si hasara kwa familia za waathiriwa pekee, bali kwa taifa zima kwa jumla. Ukichukua takwimu zilizotajwa hapa kama mfano, utaona wengi wanaohusika katika ajali hizi za wikendi ni watu ambao wangali wanategemewa kuendesha gurudumu la maendeleo katika taifa hili.
Ripoti hiyo nzima ikitumiwa vyema, nchi inaweza kufahamu sheria na sera mbazo ni dhaifu ili zibadilishwe na hatua mwafaka zichukuliwe iwapo kuna zile ambazo hazitekelezwi kikamilifu.