Makala

TAHARIRI: Timu zimakinike kutumia ufadhili

December 12th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

KITENGO CHA UHARIRI

BAADA ya wachezaji kuumia kwa muda mrefu, hatimaye kampuni ya kamari ya BetKing imeanza kutoa ufadhili wake kwa timu za soka nchini zinazoshiriki Ligi Kuu, ambayo sasa inaendeshwa na Shirikisho la Soka Kenya (FKF).

Wanasoka nchini wamekuwa wakipitia hali ngumu tangu kujiondoa kwa SportPesa waliokuwa wadhamini wakuu wa ligi, mwaka jana.

BetKing ambao sasa ndio wadhamini wa ligi walitua siku chache tu baada ya kampuni nyingine ya kamari, Betsafe, kuanza kudhamini Gor Mahia na AFC Leopards ambazo pia zilidhaminiwa kibinafsi na SportPesa.

Gor, ambao ni mabingwa mara 19 wa ligi, wanapokea Sh55 milioni kila msimu – ambao kwa kawaida huwa miezi saba. Kulingana na bajeti ya K’Ogalo, wanahitaji pesa zisizopungua Sh5 milioni kugharamia mahitaji ya kila mwezi. Itakumbukwa matatizo ya kifedha yalichangia kuondoka kwa baadhi ya wachezaji wao nyota msimu jana.

AFC Leopards nao wamekuwa wakitegemea mashabiki na wahisani kupata pesa, ambazo ziliwawezesha kuhifadhi wachezaji wao muhimu kwa msimu huu mpya.

Timu hizi vigogo wa soka nchini zilizoea kutegemea ada ya kiingilio wakati wa mechi, lakini tangu shughuli za soka zipigwe marufuku kutokana na kuenea kwa COVID-19 wachezaji wao wameumia kwa kiasi kikubwa.

Kutokana na hali hiyo, msimu ulikatizwa ghafla na Gor Mahia wakatangazwa mabingwa kwa vile ndio waliokuwa wakiongoza kwa pointi 54 kutokana na mechi 23, mbele ya Kakamega Homeboyz kwa tofauti ya pointi saba tu, wakati vijana hao kutoka Kaunti ya Kakamega walikuwa wamecheza mechi chache.

Betsafe na BetKing walikuwa wamekataa kuachilia pesa hadi mechi za msimu mpya zlipoanza rasmi wikendi mbili zilizopita.

Katika mkataba wao na Betsafe, Gor Mahia inapokea Sh55 milioni kwa mwaka wakati Leopards wakipata Sh40 milioni.

Mbali na udhamini huo wa miaka mitatu, kadhalika Afisa Mkuu wa kampuni hiyo ya karata Alex Kobia amesisitiza kujitolea kwao kusaidia kuimarisha michezo, mbali na kuendesha shughuli zao za bahati na sifu kwa utaaluma.

Tujuavyo, mchezo wa bahati na sibu una madhara yake hata kwa wachezaji na mashabiki, lakini Kobia ameahidi kuhakikisha shughuli zao zinaendeshwa kwa utaaluma wa hali ya juu, huku maslahi ya wachezaji yakizingatiwa.

Kwa uhusiano wa GamHelp Kenya, Betsafe imeahidi kupiga vita madhara ya kucheza karata, huku mwenyekiti wa GameHelp Kenya, Joseph Kamau akisema mojawapo wa njia ya kufanya hivyo ni kuhakikisha wahusika wanapata ushauri unaofaa kupitia kwa mitandao ya jamii kama SMS, WhatsApp, Skype na simu.

Alisema Betsafe inamiliki vituo vitatu vya kubadilisha tabia jijini Nairobi vijulikanavyo kama Wonderpeace Rehab Centre na Primrose Rehab na Wellness Centre ambavyo vimeajiri madaktari wa kushukulika na maswala ya kiakili na kurekebisha waliopotoshwa na mchezo wa bahati na sibu.

Betsafe ni muhimu kwa Gor Mahia na Leopards, lakini itabidi timu hizi zifatute usaidizi zaidi kwa vile pesa zinazotolewa na wadhamini wao hasitoshi kugharamia mahitaji yao ipasavyo.

Ukosefu huu wa pesa ndio ulioifanya AFC Leopards kukimbilia Galana Oil Kenya Ltd ambao waligharamia kambi yao ya mazoezi kwa wiki mbili kule Elgeyo Marakwet.

Kampuni hiyo inayoendesha shughuli zake chini ya Delta Service Stations ndio wasambazaji wa bidhaa ya ENOC Lubricants nchini Kenya.

Udhamini wa Galana umechangia pakubwa kuimarika kwa kikosi cha Leopards ambacho kilionyesha kiwango cha juu dhidi ya Tusker ligini, pamoja na mechi zingine za kujipima nguvu hapo awali.

Kutokana na hali mbaya ya uchumi nchini, mashabiki wa timu hizi wameshindwa kununua mavazi ya timu zao kama ilivyokuwa miaka ya hapo awali, wengi wakilalamika kwamba bei iliyowekwa ni ghali mno.

Hata hivyo, itakuwa vyema iwapo iwapo FKF itazikubalia timu zetu kutafuta udhamini zaidi kutoka kwa kampuni nyingine zinazotaka kusaidia vijana wetu, badala ya kuweka vikwazo vikali wakati huu Wakenya wanakabiliwa na maisha magumu.