TAHARIRI: Tuangazie sasa jinsi ya kukuza taifa letu
Na MHARIRI
WAKENYA Jumanne waliadhimisha Siku ya Mashujaa wengi wakionekana kuwaenzi na kuwakumbuka watu ambao kulingana na mtazamo wao, wamechangia jambo moja au lingine maishani mwao.
Siku hii ambayo chimbuko lake ni historia ya taifa kuhusiana na waliojitolea kupigania uhuru na ukombozi wa taifa letu, iliadhimishwa jana katika Kaunti ya Kisii.
Siku hii pia iliadhimishwa wakati ambapo taifa linaonekana kuwa na mgawanyiko hasa kuhusiana na marekebisho ya Katiba kupitia mchakato wa ripoti ya maridhiano ya BBI.
Ingawaje kufikia sasa kila mmoja anakisia tu yaliyomo, wengi wameisifu kuwa ni ripoti ambayo itasaidia taifa kwa jumla kutuliza joto la kisiasa linaloshuhudiwa nyakati za uchaguzi.
Katika hotuba yake Jumanne, Rais Uhuru Kenyatta akiongoza taifa kwa maadhimisho hayo, alihimiza kuwa huu ndio wakati mwafaka wa kufanya mageuzi kwa katiba na kuwataka Wakenya angalau wasiwe wagumu katika kufanya uamuzi huo
Hata hivyo, Rais alizungumzia haja ya maafikiano kuhusiana na harakati hizo za kubadilisha katiba. Alihimiza haja ya umoja hata wakati ambapo tunatekeleza haki yetu ya kidemokrasia.
Maoni tele yametolewa kuhusiana na dhamira halisi ya ripoti ya BBI, wengi wakiiona kuwa njama ya wachache kujifaidi wao binafsi. Lakini baadhi wameeleza kuwa inalenga kuleta suluhisho la “kunyamazisha” anayeshindwa hasa katika uchaguzi wa urais kutoambulia patupu. Ni muhimu kwa hivyo, kwa viongozi wanaohusika kuhakikisha kuwa wanaelimisha Wakenya vilivyo ripoti hii itakapotolewa ili waweze kuelewa kwa kina na kuepuka kufuata upepo.
Vile vile, litakuwa jambo la busara kwa Wakenya wenyewe kuchukua muda na kukagua ripoti hiyo kuelewa maamuzi wanayofanya na pia kuangalia ni vipi hata nao wanaweza kufaidika kimaendeleo na zaidi jinsi ya Kenya kupiga hatua na sio kushiriki siasa wakati wote.
Rais alizungumzia pia suala la usawa katika usambazaji au ugawaji wa rasilmali na nafasi pia. Wakenya wanahitaji kufikia kiwango hiki ambapo wataelekeza macho yao kwa suala la rasilmali na jinsi ya kuboresha taifa hili kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Kufanya hivyo, lazima wakome kuzingatia ukabila na urafiki ama utiifu wao kwa vyama. Ni muhimu kutambua kwamba kadri tunavyoendelea kuegemea kwa ukabila, nchi inazidi kusambaratika kwa kuwa wengi wanasalia kunung’unika na kuhisi kusahaulika hasa katika suala hilo la rasilmali na nafasi za ajira.
Ni muhimu kwa Kenya na wananchi wake kutafuta jinsi ya kuweka mikakati ya dhati ya kuboresha taifa hili liweze kufikia kiwango kingine, lau sivyo tutaendelea kupoteza fursa nyingi za kujiboresha kwa mataifa jirani baadhi ambayo yameelekeza macho yao kwa kuimarisha uchumi wa mataifa yao.