• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 7:52 PM
TAHARIRI: Tujiandae kukabili majanga ya mvua

TAHARIRI: Tujiandae kukabili majanga ya mvua

Na MHARIRI

IDARA ya kutabiri hali ya hewa tayari imetahadharisha Wakenya kuhusu msimu wa mvua utakaoanza mwezi huu.

Tahadhari hii iliwahi kutolewa mapema, na kilichofanywa sasa ni kukumbusha wananchi na wadau husika ili wahakikishe wamejiandaa vilivyo.

Kwa kawaida, ilani hizi zimekuwa zikipuuzwa na wadau wanaohusika katika masuala ya kukabiliana na janga.

Tumekuwa taifa la kusubiri majanga yatokee ndipo tutafute misaada, ilhali wakati mwingine tuna muda wa kutosha kuepusha maafa na hasara. Mvua inaponyesha kila mwaka huwa kunatokea majanga kama vile mafuriko na maporomoko ya ardhi.

Hali hizi husababisha hasara kubwa ya mali na vilevile maafa kwa wananchi walio katika maeneo hatari.

Inahitajika tuwe taifa ambalo huchukulia ilani aina hizi kwa uzito mapema na kuweka mikakati inayofaa kabla majanga yatukumbe.

Serikali huwekeza pesa nyingi mno kwa mashirika kama vile Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa, na inasikitisha jinsi kazi za idara hizo hupuuzwa.

Tunaweza kupunguza gharama kubwa ya kutoa misaada baada ya majanga ikiwa tutatilia maanani ilani za mapema.

Jukumu la kuzuia na kutatua majanga lisiachiwe serikali kuu pekee kwani pia serikali za kaunti zina jukumu kubwa.

Serikali kuu na za kaunti hutenga mamilioni ya pesa kila mwaka kutatua majanga. Pesa hizo wakati mwingine hazitoshi na huwa inalazimu nchi kutafutia waathiriwa misaada kwingineko.

Hii ni ishara tosha kuhusu gharama kubwa ya kupambana na majanga yanayoweza kuepukika.

Kando na hasara hizo zinazoweza kuonekana wazi, mafuriko huja na hasara nyingine ambazo huenda zisitambulike kirahisi.

Huo ndio wakati ambapo wananchi hukumbwa na magonjwa tele ikiwemo kipindupindu kutokana na jinsi maji yanayotegemewa na baadhi ya raia huchanganyika na majitaka.

Wakati huo pia, miundomsingi muhimu kama vile barabara na madaraja huporomoka na kutatiza sana usafiri.

Haya yote huathiri uwezo wa wananchi kuendelea kutoa mchango wao katika kuendeleza mbele gurudumu la uchumi wa nchi.

Hivyo basi, sote tutambue hasara kubwa inayotokana na majanga na tujikaze kuyazuia iwezekanavyo.

You can share this post!

Wabunge 11 wahojiwa kwa kuzuru Somalia kisiri

MATHEKA: Vijana ni hazina ya taifa, serikali iwasaidie sasa

adminleo