TAHARIRI: Turekebishe udhaifu wa kukabili majanga
Na MHARIRI
KWA siku 11 Wakenya wamekuwa wakifuatilia kwa karibu sana shughuli katika kivuko cha feri cha Likoni, Kaunti ya Mombasa.
Tangu Bi Mariam Kighenda na mwanawe watumbukie baharini pamoja na gari lao wakiwa ndani ya feri, ulimwengu mzima umekuwa ukitaka kujua kama miili yao itapatikana au la.
Kulingana na Msemaji wa Serikali, Kanali Mstaafu Cyrus Oguna, operesheni ya kusaka miili ya mama huyo na mwanawe inatarajiwa kukamilika leo Alhamisi.
Jumatano, kikosi ambacho kimekuwa kikiendeleza shughuli hiyo, kilisema kilifanikiwa kuona gari katika sakafu ya bahari.
Inatarajiwa kuwa gari hilo litatolewa kutoka baharini na kuhitimisha wiki mbili za mahangaiko kwa familia ya marehemu.
Hatimaye, msemaji wa familia iliyoathiriwa, Bw Luca Mbati anasema wamepata matumaini mapya; ya angalau kuzika wapendwa wao.
Akizungumza Jumatano, Kanali Oguna aliwamiminia sifa wanajeshi wa Majini kwa kujitolea.
Kwamba walifanya kazi kwa ujasiri mkuu bila kukata tamaa, katika eneo lililojaa samaki, mawimbi makali, giza na hata hatari ya kuishiwa na hewa safi.
Katika hotuba zote Jumatano, serikali haikuwataja wapigambizi maalum waliotoka Afrika Kusini.
Je, ina maana kuwa hawakuwa na wajibu wowote katika opereheni hiyo, sawa na walivyochukuliwa wapigambizi binafsi?
Katika tukio hili la kutumbukia kwa gari baharini, yamejitokeza mambo kadhaa yanayostahili kuwa mafunzo kwetu kama taifa.
Kwanza ni kuwa maafisa wetu waliopewa jukumu la kutulinda baharini wanahitaji mafunzo zaidi.
Kusema hivi si kuwadharau, bali kila mtu aliona jinsi ambavyo maafisa wetu walivyohangaika mno walipokuwa wakijaribu kupiga mbizi.
Serikali inapaswa iwape mafunzo maalum maafisa wa Jeshi la Wanamaji, wale wa KPA na Kenya Ferry pamoja na kikosi maalum cha kulinda fuo za bahari (Kenya Coast Guards).
Katika mataifa kama Marekani, vikosi vya baharini huweza kuokoa maisha kwa njia ya ujasiri na haraka.
Tatizo jingine ni kukosekana kwa vifaa maalum vinavyohitajika wakati wa dharura. Hata tukiwa na maafisa wenye ujuzi kiasi gani, kama hawatakuwa na vifaa bora na vya kisasa, itakuwa kazi bure.
Mkasa huu wafaa kuchukuliwa kuwa kipimo cha jinsi gani Kenya inavyopaswa kujitayarisha kwa majanga.