Makala

TAHARIRI: Ufisadi huu utaua spoti yetu kabisa

November 16th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MHARIRI

MNAMO Jumatano, ripoti ziliibuka kuwa kwa mara nyingine kikosi cha Harambee Stars kilikuwa kimezuiliwa katika hoteli moja nchini Misri ambako kilienda kukabiliana na timu ya taifa hilo katika mechi ya kufuzu kwa Kombe la Afrika (AFCON).

Kisa na maana? Timu hiyo ilikuwa imeshindwa kulipa gharama ya chakula na malazi. Aidha,ilibainika kuwa kiini cha kutolipwa kwa bili hiyo ni njama ya ufisadi miongoni mwa maafisa wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) walioandamana na timu hiyo nchini Misri.

Nakala zilizopatikana na wanahabari kuhusu bili hiyo zilionyesha kuwa hoteli ilikuwa inadai takribani Sh1.6 milioni ilhali viongozi wa FKF walikuwa wametuma vocha ya malipo kwa Wizara ya Michezo Kenya wakidai kuwa jumla ya bili ilikuwa Sh4 milioni.

Japo walidai kuwa pesa za juu zingetumiwa kulipia gharama ambazo baadhi yao walitoa mfukoni kugharimia safari ya Harambee Stars, dhahiri hii ilionyesha kuwa yupo mtu aliyekuwa na hila ya kulaghai taifa mamilioni kadhaa ya pesa.

Kwa msingi huo, serikali ilipotaka kutuma pesa hizo moja kwa moja hadi kwenye akaunti ya hoteli, viongozi hao walipinga wakisema pesa hizo zilifaa kupitia kwa akaunti tofauti ili waliokuwa wametumia gharama yao wajilipe, maadamu zingepitia hotelini, hawangerejeshewa pesa zao.

Urazini unaonyesha kuwa haiwi rahisi kwa mtu yeyote kutoa pesa mfukoni mwake atumie kwa shughuli ambayo serikali ndiyo inayofaa kugharimia. Hata wengi wasiokuwa na umuhimu kwenye ziara kama hizo huenda ili kunufaika kwa kuvinjari pamoja na kumegewa sehemu ya pesa inazotoa serikali.

Kwa hivyo, pana uwezekano mkubwa kuwa hakuna aliyetumia pesa zake binafsi kugharimia ziara hiyo ya Harambee.

Hili siyo tukio la kwanza linaloaibisha taifa katika medani ya kimataifa; pamewahi kutokea mipangilio mibaya na nyendo zisizofaa timu hii ikienda kucheza nje ya nchi; ikiwemo hata kukwama njiani baada ya ndege inayofaa kuisafirisha timu kukosa kulipwa.

Wala tukio hili si kwa Harambee Stars tu bali pia kwa klabu na timu za michezo mingineyo kama vile kikosi cha Kenya cha Olimpiki cha Rio, timu ya taifa ya netiboli iliyokwama Afrika Kusini majuzi, Gor Mahia ilipokuwa inaelekea kwa mechi ya CAF kule Afrika Magharibi mwaka jana na matukio mengine ya nui hiyo.

Jibu ni lipi? Sharti hatua kali zichukuliwe kuzima ufisadi hasa ndani ya FKF pamoja na katika Wizara ya Michezo, nayo wizara hiyo yafaa ihakikishe kuwa pana mipango mizuri inayofanywa mapema kabla ya timu yoyote ya taifa kuondoka kwenda kufanyia taifa kibarua nje ya nchi.